Tumeshuhudia Yanga ikipoteza mechi yake ya pili kati ya tatu ilizocheza kwenye kombe la shirikisho Afrika. Yanga imekubali kichapo cha magoli 4-0 ugenini dhidi ya Gor Mahia kwenye uwanja wa Kasarani Nairobi-Kenya.
Imefungwa idadi ya magoli manne ambayo ilifungwa kwenye mechi yake ya kwanza ilipocheza ugenini dhidi ya USM Ulger ya Algeria.
Kuna sababu nyingi kwa Yanga kupoteza mechi yao dhidi ya Gor Mahia lakini www.shaffihdauda.co.tz imeangazia maeneo matatu.
Kiufundi.
Kwa tulichokiona tunaweza kusema Yanga hwakujiandaa lakini Gor Mahia walijiandaa. Kwenye michezo haijalishi ni soka, masumbwi au kikapu, maandalizi ni kufanya majaribio uwanjani sio mazoezi tu bila mechi za kujipima.
Huwezi kuwa umejifungia unafanya mazoezi halafu ukasema unajiandaa, Gor Mahia walikuwa na faida zote, ligi ya Kenya inaendelea, wana kikosi kipana kwa sababu waliweza kukigawanya kuna kikosi kilikuja kwenye Kagame Cup kingine kilibaki Kenya.
Yanga walikaa karibu mwezi na nusu bila mechi za ushindani tangu walipotolewa kwenye michuano ya SportPesa nchini Kenya, kwa hiyo wavhezaji hawawezi kuwa katika hali ya ushindani.
Mechi ilikuwa kati ya timu iliyojiandaa dhidi ya timu ambayo haijajiandaa na kama Gor Mahia wangekuwa makini zaidi wangefunga magoli zaidi ya manne kwa sababu walikosa mabao ya wazi kama mawili au matatu.
Kisaikolojia
Hakuna asiyefahamu kwa sasa Yanga wanapitia kipindi kigumu kuna mambo mengi ambayo alizungumza ofisa habari wa timu Dismas Ten ambayo hayahitaji elimu kubwa kutambua kwamba ndani ya Yanga mambo hayapo sawa.
Kukosekana kwa wachezaji wenye ubora na uzoefu.
Tambwe amekosekana kwenye kikosi cha kwanza kwa kipindi kirefu sana, Yanga imemkosa Kamusoko mwenye ubora kwa muda mrefu, wamempoteza Chirwa na Ngoma, Yondani, Kessy hawakuwepo.
Ukiangalia profile ya wachezaji ambao wamekosekana na ambao walicheza dhidi ya Gor Mahia unapata picha halisi ya matokeo waliyopata.