Sakata la Fei Toto kusaini Yanga, Singida lilivyokuwa


YANGA, jana iliwatambulisha nyota wawili wapya, Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ kutoka JKU ya Zanzibar iliyompa mkataba wa miaka mitatu na Jaffar Mohammed aliyekuwa Majimaji aliyepewa mkataba wa miaka miwili. 

Katika usajili huo, gumzo kubwa lilikuwa ni usajili wa Fei Toto ambaye kabla ya jana jioni Yanga haijamtangaza kuwa mchezaji wao, asubuhi yake, Singida United ilimtambulisha imemsajili kwa kumpa mkataba wa miaka mitatu. 

Usajili huo ilikuwa kama filamu kwani asubuhi Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, alitangaza wamemsajili mchezaji huyo na kusambaza picha pamoja na video zinazoonyesha uthibitisho wa hicho kilichofanyika. 

Haikupita muda mrefu, jioni Yanga ikamtambulisha Fei Toto klabuni kwao ambapo katika utambulisho huo, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika ndiyo walihusika. 

Mbali na Singida kutangaza kumsajili Fei Toto kabla ya Yanga haijapindua meza kibabe, Simba nayo inatajwa ilikuwa ikimuhitaji mchezaji huyo na ilibakia kidogo wampe mkataba, ikashindikana. 

Akizungumza na Championi Ijumaa mara baada ya kukamilisha usajili huo, Nyika alisema: “Ndiyo tumeanza kazi katika usajili wetu, tulianza na Mohammed Banka, leo (jana) tumemalizana na wachezaji hawa wawili. 

“Usajili huu tunaufanya kwa weledi mkubwa tukifuata matakwa ya mwalimu wetu Mwinyi Zahera kwani aliagiza anataka tuimarishe kwenye nafasi ya kiungo na hata ukiangalia, Fei Toto, Jaffar na Banka, wote wanacheza nafasi hizo.” 

Naye Meneja wa JKU ambaye pia ni meneja wa Fei Toto, Mohammed Kombo ‘Afande Chimoudy’, alimaliza utata kwa kusema: “Kuanzia leo (jana Alhamisi), Feisal ni mchezaji rasmi wa Yanga baada ya kumalizana nao kwa kila kitu. 

“Licha ya Singida kutangaza wamemsajili, lakini hawezi kuwa mchezaji wao kwa sababu walishindwa kufuata utaratibu, wao waliongea na mchezaji mwenyewe wakashindwa kutufuata sisi viongozi. Jambo kama hili lililofanywa na Singida halikubaliki na ingekuwa kuna uwezekano timu kama hizi zikafungiwa.” 

Kwa upande wa Fei Toto, alisema: “Kuanzia sasa mimi ni mchezaji wa Yanga na naahidi nitafanya makubwa ndani ya timu hii. Ni kweli Singida na Simba walinifuata lakini nimeamua kuja Yanga kwa sababu nimeona ndiyo sehemu sahihi kwangu.” 

Wakati hayo yakijiri, taarifa kutoka Simba zinasema kuwa, walikuwa wamekaribia kumsajili Fei Toto ambapo walimtengea kitita cha Sh milioni 30 na mshahara wa Sh milioni mbili pamoja na gari, lakini mchezaji huyo alishindwa kusaini Simba baada ya vigogo wa Yanga kumficha nyota huyo. 

Singida waja juu 
Baada ya utambulisho huo wa Yanga, Mkurugenzi wa Singida United alitoa tamko kwa kusema: “Feisal tumemsaini kwa mkataba wa miaka mitatu tukiwa tumekutana naye chini ya mwanasheria na wakala wake na mchezaji mwenyewe alikubali kusaini na sehemu kubwa ya fedha ameshachukua. 

“Hajasaini ‘pre contract’ kama watu wanavyosema, ile ni ‘contract’ inayotambulika na ndiyo itatumika kwenye usajili wake kama ambapo tutakuwa tumefikia makubaliano ya kumsajili pale TFF watakapoamua. 

“Sisi tunajua mchezaji huyu amesajili Singida United, haya ambayo yametokea kwamba amesajili Yanga ni ‘double standards’ kwa sababu linawaweka Watanzania njia panda. Sisi tunaamini vyombo vinavyohusika na usajili ambavyo ni Bodi ya Ligi na TFF vitaamua jambo hili kwani tumeshamalizana na JKU.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad