Waziri wa Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola amekutana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Sirro na maofisa wengine wakuu wa Jeshi la Polisi, Makao makuu ya Polisi DSM.
Alisema hadi juzi saa 12 alihitaji maelezo hayo ambayo mpaka jana jioni Julai 20, 2018 hayajatolewa.
Lugola alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuona utendaji kazi wa jeshi la polisi bandarini hapo.
Amesema alibaini kati ya mbwa sita maalum, wawili wapo mafunzoni na wanabaki wanne ambapo kati yao mmoja aitwaye Hobby hajulikani alipo.
Mapema jana mtandao wa MCL Digital ilizungumza na waziri huyo na kubainisha kuwa mbwa wengine 30 wametoroshwa katika kikosi cha farasi na mbwa bandarini hapo.
Amesema mbwa anayesakwa kwa sasa, bado hajapatikana, “nilivyoenda kikosi cha farasi na mbwa jana nilibaini madudu zaidi tofauti na nilivyotarajia. Siyo mbwa huyu tu Hobby nimebaini mbwa wengine zaidi ya 30 wametoroshwa na taarifa nilizo nazo wameanza kurejeshwa kimya kimya.”
Amesema atafanya kikao na IGP Sirro na baadaye atazungumza na maofisa waandamizi wa polisi.
“Kikao hiki kitakuwa na ajenda mbalimbali ikiwamo kutaka kujua sakata la mbwa hao,” amesisitiza.