RAIA wa Italia, mwenye umri wa miaka 46 amezuiliwa Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume visiwani hapa na kurudishwa nchini mwake baada ya kubainika kuwa amebadilisha jinsia yake.
Mtu huyo aliingia Zanzibar wiki hii alibainika kubadilisha jinsia na kwamba katika hati yake ya kusafiria ilionyesha mwanaume, lakini yeye alionekana kama ni mwanamke baada ya kujibadilisha.
Akizungumza na Nipashe, Ofisa Uhusiano wa Idara ya Uhamiaji, Mlalama Amlima, alisema raia huyo ambaye alijulikana kwa Davide Katena alifanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa ni mwanaume ingawa alivaa mavazi ya kike.
Alieleza kuwa, walianza kumtilia mashaka baada ya kushuka uwanjani hapo na walipojiridhisha kuwa ni mwanamme akazuiliwa kuingia nchini na kulazimika kurejea alikitoka.
Aidha, alisema raia huyo ambaye alikuja Zanzibar na Shirika la Ndege la AAKIA majira ya saa tisa alfajiri ya kuamkia jumatano na tayari amesharejea nchini kwao.
Alisema kuwa raia huyo ni msanii na alikuja Zanzibar kwa ajili ya kufanya maonesho ya muziki.
“Tulipojaribu kumuhoji raia huyo pia alisema kuwa ana jina la kike ambalo ni Cristina Bugatty ambalo anatumia katika sanaa,” alisema.
Alieleza kuwa wamemzuia kuingia nchini kutokana na kitendo alichokifanya ni kinyume na sheria na taratibu za uhamiaji.
“Ujio wa raia huyo ungevuta taswira ya ukahaba nchini kinyume na sheria, silka na desturi za jamii ya Kitanzania,” alisema.
Hata hivyo, alieleza kuwa hilo sio tukio la kwanza kuwarejesha raia kama hao ambao wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja na wengine hufika Zanzibar kwa ajili ya fungate baada ya nchini kwao kufunga ndoa.