Shule ya Kata iliyoongoza kitaifa hii


Kumekuwa na imani tofauti juu ya suala zima la elimu bora, wapo wanaoamini katika fedha kuwa ndio chanzo cha ufaulu kwa wanafunzi, kuna wanaoamini bidii na utayari wa mwanafunzi na wengine wanaamini katika uhodari wa walimu na wanafunzi. 

Shule ya sekondari ya Kisimiri, ni miongoni mwa shule 10 zilizofanya vizuri kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita, shule hiyo ni ya Kata na inapatikana mkoani Arusha wilayani Arumeru katika kijiji cha Kisimiri. 

Mmoja kati ya walimu mwanzilishi wa shule hiyo, Mwalimu Emanuel Kisongo John ambaye kwa sasa ni  Afisa Elimu mkoa wa Mara, amezungumza na Weekend BreakFast ya East Africa Radio, ambapo amesema kuwa haikuwa 
rahisi kuifikisha shule hiyo katika matokeo hayo kutokana na jiografia ya eneo hilo lililozungukwa na jamii ya wafugaji na ndoa za utotoni. 

Mwalimu Kisongo amesema kuwa mwalimu bora lazima uweze kubadili mitazamo ya jamii, na kuongeza kuwa ufaulu wa wanafunzi hauhitaji ada kubwa wala ubora wa majengo tofauti na wengi wanavyodhani. 

"Mwalimu anapelekwa shuleni ili kusaidia wale wasiojiweza, huwezi kuwa mwalimu kama huwezi badili mtazamo wa jamii, huwezi kuwa mwalimu halafu unadai wingi wa wanafunzi ndio chanzo cha matokeo mabovu mbona wachina ni wengi lakini ndio wanatuongoza katika teknolojia", amesema Mwalimu Kisongo. 

Shule hiyo mwaka juzi ilifanikiwa kushika nafasi ya kwanza, mwaka jana ilifanikiwa kushika nafasi ya tatu,  na mwaka huu imeshika nafasi ya pili kitaifa, mbali na imani ya wengi iliyojengeka kuwa shule za kata hazifanyi vizuri. 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad