Simba ni kama imeshtukia vile ni baada ya benchi la ufundi la timu hiyo kuuomba uongozi umsajili beki mwingine wa kati mwenye uzoefu na uwezo mkubwa kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Timu hiyo chini ya mfadhili wake bilionea, Mohamed Dewji ‘Mo’, inataka kusajili beki mwingine ikiwa ni siku chache tangu imlete Muivory Coast, Pascal Serge Wawa anayeichezea timu hiyo katika michuano ya Kombe la Kagame.
Kwa mujibu wa gazeti la Championi, limeeleza kuwa timu hiyo huenda ikamshusha beki mwingine kutoka Ghana au Nigeria ambapo punde atakapotua tu atasaini mkataba moja kwa moja baada ya kujiridhisha.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, uongozi wa timu hiyo bado haujaridhishwa na safu yao ya ulinzi na haraka umechukua maamuzi ya kusajili beki mwingine mmoja wa kati kabla ya dirisha kufungwa Julai 26, mwaka huu.
Chanzo hicho kilisema, uongozi umejiridhisha hilo katika michuano ya Kombe la Kagame inayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa, Uhuru na Azam Complex jijini Dar es Salaam.
“Benchi la ufundi limebaini upungufu kwenye safu ya ulinzi, hivyo ni lazima tusajili beki mwingine wa kati mwenye uzoefu na uwezo mkubwa kabla ya usajili wa ligi kufungwa.
“Kama unavyofahamu sisi Simba malengo yetu siyo ubingwa wa ligi pekee, tunataka kuona timu yetu ikifika mbali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika tutakayoshiriki, mwaka huu mwishoni,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Mrundi, Masoud Djuma kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Mimi sihusiki katika kusajili, mimi nahusika katika kutoa mapendekezo pekee ambayo nilishayakabidhi kwa uongozi ambao wao wanayafanyia kazi hivi sasa.”