Mbunge wa Iringa Mjini Mch. Peter Msigwa, amedai kwamba mabadiliko ya kumtoa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt Mwigulu Nchemba na kuteuliwa Mh. Kangi Lugola hayawezi kubadili chochote ndani ya wizara hiyo isipokuwa uchochezi.
Akizungumza na www.eatv kuhusiana na mabadiliko madogo yaliofanyika katika baadhi wizara mwishoni wa wikiiliyopita, Mh. Msigwa amesema hakuna chochote atakachokifanya Kangi isipokuwa maneno mengi yanayoweza kumfurahisha mkuu wake.
"Sitegemei kuona mabadiliko yoyote kwenye wizara hii zaidi ya uchochezi. Kangi ana maneno mengi ambayo yataweza kumfurahisha mkuu wake wa kazi lakini si mabadiliko. Lugola huwa ni mti wa kugeuka geuka hivyo atakuwa mtu wa vichekesho 'so' sioni mabadiliko" Msigwa.
Akiuzungumzia utawala wa Mwigulu Nchemba ambaye alichukua wizara hiyo kutoka kwa Charles Kitwanga, Msigwa amesema hakuna alichokifanya katika Wizara hiyo zaidi ya kusaidia kuzuia mikutano ya kijamii pamoja na kanuni za nchi.
"Mwigulu hajafanya chochote katika wizara, kuwepo au kutokuwepo kwenye wizara sitaona tofauti yoyote. Kwenye Wizara ile Mwigulu alikuwa kama picha kwani katika kipindi chake ndipo ajali za barabarani zimeongezeka, watu wameokotwa kwenye viroba, Mauaji yameongezeka, amesaidia sana kuzuia mikutano ya vyama".
Ameongeza kwamba "Mwigulu alikuwa anashadadia mambo ya hovyo yanayokwenda tofauti na katiba ya nchi na kanuni za nchi. Sioni tofauti yake".