Chuo cha Kilimo SUA Kimefanya utafiti na kubaini kuwa mbegu za matunda zinaweza kutibu matatizo ya nguvu za kiume na mzunguko wa hedhi uliovurugika kwa mwanamke.
Katika miaka ya karibuni wanaume wengi wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo la kukosa nguvu za kiume na kusaka tiba bila mafanikio huku wengine wakikimbilia kwa waganga wa kienyeji.
Hivyo wanafunzi wa SUA wakachukua fursa hiyo kuja na mbinu mbadala ya kukomesha tatizo hilo ambapo wamegundua kwamba mbegu za matunda kama tikitikimaji, maboga, alizeti, papai na matunda mengine zinaweza kutibu matatizo hayo.
Stewart Mwanyika ambaye ni Mtafiti Mwandamizi kutoka SUA amesema kiasili mbegu zina kiasi kikubwa cha madini ya zinki ambayo yanachangia kutengeneza homoni na chembechembe zinazohusika na utendaji bora wa via vya uzazi hasa vya mwanaume.
Hivyo ameshauri watu kutumia mbegu hizo mara kwa mara iwe tiba ya kudumu kwani madini ya zinki yanatengeneza haraka chembechembe nyeupe za damu ambazo ni kinga ya mwili na seli nyingine zinazohusika na via vya uzazi.
”Ukila matunda kama tikitimaji usitupe mbegu, tafuna meza na kama harufu inakukera unaweza kuzitoa na kuzikausha kisha oka ili kuongeza ladha kisha tafuna, mbegu za papai pia ukiweza kuzila ni vizuri lakini zina uchungu, ila kwa mbegu za alizeti na maboga kuzikaanga kisha unatafuna unameza” amesema Stewart.