Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba jana usiku amefanya ziara ya kushtukiza katika maduka makubwa ya kuuza na sukari na mchele jijini Dar es salaam,na kubaini kuna uingizwaji wa bidhaa hiyo kimagendo na kutoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuwakamata wahusika.
Waziri wa Kilimo akiambatana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Miraji Kipande amesema kuwa uuzwaji wa bidhaa hizo unahitaji mfanyabishara kufuata na kukamilisha utaratibu , hivyo wafanyabiashara wanaouza sukari na mchele kinyume cha sheria, Kanuni na taratibu za nchi wawajibishwe mara moja.
Katika ziara hiyo Waziri amekuta Sukari na mchele uliokuwa ukiuzwa na wafanyabiashara hao kinyume na taratibu za nchi, Sukari iliyokutwa ilikuwa imefungashwa katika ujazo wa kilo moja moja na zilisomeka kuwa zimetoka nchini Mauritius na Uingereza ambazo ziliingizwa nchini bila ya kuwa na kibali cha Waziri Mkuu au Bodi ya Sukari Tanzania ambayo ipo chini ya Wizara ya Kilimo.
Kwa sasa wafanyabiashara hao wametiwa nguvuni na suala hilo limefikishwa Polisi kwa ajili ya uchunguzi na taratibu zingine za kisheria pindi uchunguzi utakapokamilika watuhumiwa hao watapandishwa kizimbani.