Idara na taasisi za serikali zimeagizwa kuialika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwenye mikutano yao ili itoe mada kuhusu elimu ya masuala ya rushwa, lengo likiwa ni kupunguza na kuondoa rushwa kwa watumishi wa Umma.
Maagizo hayo yametolewa jijini Dar es Salaam, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, wakati akizungumza na watumishi wa umma, kwenye siku Maalum ya Mapambano dhidi ya Rushwa, iliyoadhimishwa kwenye Maonyesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara jijini Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba.
“Watumishi wa Umma nchini tekelezeni wajibu wenu ipasavyo katika mapambano dhidi ya rushwa ili kuliwezesha taifa kufikia lengo la uchumi wa viwanda”, amesema Mkuchika.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, amesema kwa mara ya kwanza katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam mwaka huu, imetengwa siku maalum ya mapambano dhidi ya rushwa, lengo likiwa ni kusambaza ujumbe wa elimu ya rushwa.