Takukuru Yachunguza Miradi ya Bilioni 15 Rukwa

Takukuru Yachunguza Miradi ya Bilioni 15 Rukwa
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Rukwa, inaifanyia uchunguzi miradi minne yenye thamani ya Sh. bilioni 15.3 iliyotekelezwa kwa kukiuka sheria ya manunuzi na kuisababishia hasara serikali.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi jana ofisini kwake mbele ya waandishi wa habari ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu, Mkuu wa Takukuru mkoani humo, Hamza Mwenda, alisema uchunguzi huo upo katika hatua za mwisho kukamilika ili watuhumiwa waweze kufikishwa mahakamani.

Alisema uchunguzi uliofanywa mpaka sasa, umebaini kuwapo kwa upungufu mkubwa unaojirudia katika mchakato wa manunuzi, usimamizi wa mikataba na malipo kwa miradi ya umma ambayo yameilazimisha taasisi hiyo kuchukua hatua.

Mwenda aliyataja baadhi ya upungufu uliosababisha taasisi hiyo kuchukua ni pamoja na kutoandaliwa kwa ukamilifu vitabu vya zabuni wakati zabuni husika ikitangazwa.

Alisema baadhi ya zabuni zimekuwa zikitangazwa katika magazeti yasiyo na mzunguko mkubwa ama wasomaji wengi au kutangazwa katika magazeti yanayotoka mwisho wa wiki ambayo hayawafikii wasomaji ipasavyo.

Mkuu huyo wa Takukuru, alitaja upungufu mwingine kuwa ni kutofautisha kurasa yenye maelezo ya msingi ya mkataba ikiwamo bei kutofautishwa na kurasa inayotiwa saini, hali inayosababisha uwezekano wa kubadilishwa kwa taarifa za mkataba bila watia saini kuhusishwa.

Alisema taasisi hiyo imebaini kuwa baadhi ya kazi zimeanza kutekelezwa kabla hata ya mkataba husika kusainiwa kitendo kinacho kinaashiria kuna kupeana kazi kienyeji bila kufuata sheria inavyotaka.

Mwenda alisema hizo ni sababu chache miongoni mwa nyingi zinazo sababisha Takukuru kufanya uchunguzi katika miradi hiyo minne kwa kuwa kuna kila dalili ya ukiukwaji wa sheria na rushwa hali ambayo haiwezi kufumbiwa macho kutokana na kuitia serikali hasara kubwa.

Hata hivyo, aliwataka watumishi wa umma bila kujali nafasi zao, pamoja na wazabuni kuwa waadilifu na kuzingatia sheria mbalimbali  tofauti na hivyo wengi wao watafikishwa mbele ya sheria.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad