Kampuni ya Ulinzi inayojulikana kwa jina la 'Kiwango Security' imewaondoa wafanyakazi wake wote katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa madai ya kuwa haijalipwa fedha zake.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Uendeshaji wa Kampuni hiyo, Sunday Marwa, amefunguka na kusema wanaidai TFF kiasi cha fedha zaidi ya milioni 50 za kitanzania ambazo zinapaswa kulipwa ili huduma ya walinzi kufanya kazi iendelee.
Marwa amesema wameamua kufanya hivyo kwa maana deni lingekuwa kubwa na hivyo imewabidi wafanye hivyo ili lisizidi kuongezeka.
“Kampuni imefikia hatua ya kufanya maamuzi hayo kutokana na walinzi wetu kuzidi kufanya kazi katika ofisi ambazo haziwalipi chochote, jambo ambalo sisi kama ofisi tumeona ni kuwatesa bure wafanyakazi wetu”, amesema Marwa.
Mbali na ofisi hizo, Marwa amesema Kiwango Security iliingia mikataba miwili na TFF ambapo walinzi walikuwa wanazilinda ofisi za TFF pamoja na kwenye makazi ya Rais wa Shirikisho hilo Wallace Karia.
Www.eatv.tv imeutafuta uongozi wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), ili kujibu tuhuma hizo lakini hawakuonesha ushirikiano.