Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umesema kauli ya Rais John Magufuli aliyoitoa jana, akitaka wafungwa kutumikishwa wakiwa gerezani, inakiuka Katiba ya nchi na haki za binadamu.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla fupi ya kumuapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike na Balozi Joseph Sokoine ambaye ameteuliwa kuwa naibu katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Rais Magufuli alimtaka Kasike kuhakikisha wafungwa wanafanya kazi ipasavyo, wazuie matumizi ya simu gerezani, washiriki katika shughuli za kilimo na ujenzi, wazuie kufanya biashara na kushiriki katika matukio ya wizi wakiwa gerezani na wazuie kujamiiana.
“Unakuta hata maaskari na watumishi hawana nyumba za kukaa na wafungwa wapo tena wa bure kabisa ambao unaweza kuwaambia wafyatue matofali na teke ukawapiga. Askari huna pa kulala na wafungwa wapo, lakini unawatafutia Bajeti ya Serikali,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumza na MCL Digital leo Jumapili Julai 15, 2018 mkurugenzi wa mtandao huo, Onesmo Ole Ngurumwa amesema, “mfungwa ana haki ya kula na kuishi na wakati mwingine anaweza kufanya shughuli akiwa gerezani ambazo zitamuingia kipato na hizo fedha akatunziwa na kupewa siku akitoka gerezani ili zimsaidie,”
“Mgungwa anapaswa kupata haki zake za msingi na haimaanishi mtu akiwa mfungwa apigwe, anyanyaswe na kufanya hivyo ni kwenda kinyume na haki za binadamu. Mfungwa hapaswi kupigwa na hakuna sehemu yoyote inasema apigwe na kunyanyaswa.”
Amesema kauli kwamba mfungwa apigwe, afanye kazi na kugeuzwa kitega uchumi inashtua na ni kinyume na Katiba na haki za binadamu.
Chanzo: Mwananchi