Baraza la vyama vya michezo Afrika Mashariki na kati CECAFA limeifungia klabu ya Gor Mahia kushiriki michuano ya Kagame Cup kwa muda wa miaka miwili.
Adhabu hiyo imetangazwa na Katibu mkuu wa CECAFA, Nicolas Musonye kwenye mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam hii leo.
Baada ya kuifunga klabu ya JKU katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa michuano hiyo ya Kagame, Gor Mahia iligoma kwenda kuchukua medali zake na kuamua kuondoka.
Waandaaji wa mashindano hayo walilazimika kuiita klabu ya Simba jukwaani baada ya kuisubiri Gor Mahia kwa takribani dakika tano bila mafanikio.
“Tuliandaa kila kitu kwaajili ya utoaji wa zawadi lakini Gor Mahia hawakutokea katika tukio, mbali na hilo pia walipofika hapa walikataa hoteli, waligomea vyumba vya kubadilishia nguo na jana hawakutokea mbele ya wageni wetu “.
“Pia tumemuonya kocha wa Gor Mahia (Dylan Kerr) kwa kuwatolea lugha chafu makamisaa wa mchezo na tumeshalitaarifu shirikisho la soka Kenya (FKF) , lakini kwa sisi hawatoshiriki mashindano ya Kagame Cup kwa miaka miwili ijayo “. Amesema Musonye.
Mashindano hayo yamemalizika kwa Azam Fc kuibuka washindi baada ya kuifunga Simba 2-1 na kufanikiwa kuutetea ubingwa huo ambao katika mashindano yaliyofanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2015.