Rais wa Marekani Donald Trump anakusudia kumwalika Washington, Rais wa Urusi Vladmir Putin baadaye mwaka huu, licha ya kuendelea kuwepo ukosoaji juu ya mkutano wao uliofanyika Jumatatu wiki hii katika mji mkuu wa Finland Helsinki.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sara Sanders amesema majadiliano kuhusiana na ziara hiyo tayari yameanza.
Hata hivyo, Kiongozi wa maseneta kupitia chama cha Democrat nchini humo Chuck Schumer ameupinga mualiko huo mara moja kwa kusema kuwa Rais Trump hapaswi tena kukutana ana kwa ana na Rais Putin mpaka pale Wamarekani watakapojua nini kilitokea katika mkutano wa Helsinki.
Awali katika mkutano wake na kituo cha televisheni cha CNBC Rais Trump alitetea tena msimamo wake wa kuimarisha mahusiano na Urusi, lakini amesema kama jambo hilo halitafanikiwa, atakuwa adui na Rais huyo wa Urusi kushinda ilivyokuwa awali.
Wakati huohuo taarifa hizo za mualiko wa Rais Putin, zimeonekana kumshangaza Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Marekani Dan Coats, ambaye aliambiwa jambo hilo katika mahojiano ya moja kwa moja wakati wa mkutano wa usalama uliofanika katika jimbo la Colorado.
Ameongeza kusema kuwa bado hajafahamu nini walichojadili Rais Putin na Trump katika mkutano wao, ambao ulihudhuriwa tu na watafsiri wao.