Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imependekeza mambo mawili muhimu ya mienendo ya uendeshaji wa kesi mahakamani, ikiwamo kitambulisho cha Taifa kutumika kudhamini mtu. Jambo jingine ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutofuta kesi siku ya hukumu.
Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na katibu mtendaji wa tume hiyo, Casmir Kyuki wakati akikabidhi taarifa mbili kwa waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.
Taarifa hizo ni za mapitio ya mfumo wa sheria wa utoaji huduma za ustawi wa jamii na ya sheria kuhusu utoaji haki jinai.
“Tume inapendekeza mahakama itumie vitambulisho vya Taifa wakati wa kutoa dhamana kwa makosa yenye dhamana ili kuondoa ulazima wa utambuzi wa viongozi wa serikali za mitaa au mwajiri,” alisema Kyuki.
Alisema kumekuwapo na changamoto kwa watuhumiwa kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana kwenye kesi ambazo dhamana ziko wazi.
“Tume inapendekeza kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kirekebishwe ili kumpatia mtuhumiwa haki ya kusikilizwa pale Mkurugenzi wa Mashtaka anapotoa hati ya kupinga kutolewa kwa dhamana,” alisema Kyuki.
Akigusia suala la DPP kufuta kesi siku ya hukumu, alisema tume inapendekeza kifungu cha 91 cha sheria hiyo, sura 20 kifanyiwe marekebisho ili kumtaka DPP aweze kuondoa shauri mahakamani kabla upande wa utetezi haujaanza utetezi wake.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hizo, Profesa Kabudi aliitaka tume hiyo kuainisha maeneo yote ambayo sheria zake zina matatizo. Pia alisema ameyapokea mapendekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.