Ufafanuzi Kuhusu Upotoshwaji Wa Bei Za Mafuta


1. UTANGULIZI
Moja ya majukumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika kudhibiti sekta ndogo ya mafuta ni pamoja na kushamirisha ushindani kwa kuweka mizania sawa ya ushindani; na kumlinda mtumiaji wahuduma. Katika kutimiza jukumu hili, EWURA hukokotoa bei kikomo za mafuta kwa nchi nzima ikizingatia gharama halisi za uagizaji wa mafuta ambazo hujumuisha bei ya mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji, kodi na tozo mbalimbali za serikali, faida ya wafanyabiashara na gharama za usafirishaji ndani ya nchi.

Kwa sasa mafuta yanapokelewa katika Bandari za Dar es Salam, Tanga na Mtwara, hivyo kuchochea uwepo na tofauti za bei Kikomo. Bei hizo kikomo hutangazwa kila Jumatano ya kwanza ya mwezi kwa kutumia kanuni maalum (Petroleum Pricing Setting Rules) iliyopitishwa kwa mujibu washeria. 

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, bei yamafuta katika soko la dunia inayotumika katikakukokotoa bei ya mafuta kwa mwezi husika hapanchini ni ile ya miezi miwili ya nyuma kabla ya mafuta hayo kuanza kutumika. Kwa Mfano, bei za mafuta hapa nchini kwa mwezi Agosti, 2018 zita kokotolewa kwa kuzingatia bei zamafuta katika soko la dunia za mwezi Juni, 2018.

2. KIINI CHA TOFAUTI ZA BEI YA MAFUTA KATI YA DAR ES SALAAM NA TANGA KWA MWEZI JULAI 2018

Bei za mafuta kwa mwezi Julai 2018 zimeonekana kuwa na tofauti kubwa kati ya mafuta yaliyoingizwa nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam na ile ya Tanga. Tofauti hiyo ya bei za mafuta inatokana  na sababu mbili kama zilivyoelezwa hapa chini-:

(a) Shehena zote za mafuta ya Petroli na Dizeli inayotumika kwa sasa ilikokotolewa kwa bei ya soko la Dunia la Mei 2018, bei ambazo kimsingi zimepanda kutokana na bei za soko la dunia kwa Mwezi Mei kupanda.

(b) Tofauti na mafuta yaliyopokelewa bandari ya Dar es Salaam, Mafuta Bandari ya Tanga kwa mara ya Mwisho yalinunuliwa Mwezi Aprili, 2018, ambapo bei zake katika soko la Dunia la Machi, 2018 ilikuwa haijapanda kama ilivyopanda kwa Mwezi Mei, 2018.

Kwa kuwa Tanga wameendelea kutumia mafuta yaliyoingizwa Machi, 2018, bei zake zimekuwa za chini ikilinganishwa na mafuta yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam. (Mara ya mwisho kukokotoa bei ya mafuta yaliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga ilikuwa mwezi Mei, 2018, na bei hiyo ilikokotolewa kwa kuzingatia kuwa mafuta hayo yalinunuliwa kwa bei ya soko la dunia ya mwezi Machi 2018.)

Bei ya reja reja kwa mkoa wa Tanga ni Sh 2,234/lita kwa Petroli na Sh 2,168/lita kwa  Dizeli, wakati kwa mkoa wa Dar es Salaam ni Sh 2,409/lita kwa Petroli na Sh 2,329/lita kwa Dizeli. Hivyo bei za mafuta kwa mkoa wa Tanga ziko chini kwa kiasi cha Sh 175/lita kwa Petroli na Sh 161/lita kwa  Dizeli ukilinganisha na bei za mkoa wa Dar es Salaam. Kwa sababu hiyo mafuta ya Tanga yamekuwa na bei ya chini kuliko yanayotokea Bandari ya Dar es Salaam.

3. ONYO:

EWURA inatoa onyo Kali kwa wote wanaosambaza habari za kupotosha kwa suala hili kwani kinachofanyika ni kutaka kuvuruga soko hatua ambayo itatafsiriwa kama ni uhujumu uchumi. Hivyo basi atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.

IMETOLEWA NA:
Idara ya Mawasiliano na Uhusiano
Julai 26, 2018
Dodoma.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad