Uongozi wa klabu ya Yanga umesema hautaweza kuwatumia wachezaji wake wapya waliowasajili hivi karibuni kwenye mechi yake ya leo dhidi ya Gor Mahia ya nchini Kenya kutokana na kutokamilisha usajili wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Hayo yamebainishwa na Afisa habari wa Yanga, Dismas Ten na kuwataja wachezaji hao kuwa ni Deus Kaseke, Mrisho Ngasa pamoja na Mohamed Banka huku akifafanua zaidi kuwa sababu kubwa ni kutokamilika kwa baadhi ya vitu kwenye usajili wao.
"Kulitokea changamoto kwenye mfumo wa usajili hivyo hatutaweza kuwatumia wachezaji hao licha ya kuwa walitakiwa kujumuishwa kwenye mashindano ya kimataifa", amesema Dismas.
Pamoja na hayo, Dismas ameendelea kwa kusema "kucheza na Gor Mahia ni changamoto kwa maana kwamba Gor ni timu nzuri na yenye matokeo mazuri wakati wote. kwenye michezo kadhaa waliowahi kucheza hivi karibuni tumeona jinsi wanavyocheza, nasi pia tumefanya mazoezi ya kutosha lengo ni kuona timu inakaa sawa sawa kwaajili ya huu mchezo wa leo ambao unapopata matokeo unaweza kujitengenezea nafasi nzuri kwenye msimamo wa kundi kabla ya kwenda kwenye hatua nyingine".
Yanga itashuka dimbani majira ya saa 1:00 usiku kuvaana na Gor Mahia ambapo baada ya mchezo wa leo timu hizo mbili zinatarajiwa kurudiana tena Jijini Dar es Salaam Julai 19 mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa.