Usajili Wamkera Mourinho


Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ameonesha kutofurahishwa na utendaji wa bodi pamoja na mkurugenzi mkuu wa klabu hiyo juu ya usajili uliofanywa kuelekea msimu mpya wa mashindano. 

Mourinho amefunguka kuwa angependa akamilishiwe usajili wa wachezaji wake anaowahitaji ili kuimarisha kikosi kabla ya dirisha la usajili kufungwa Agosti 10 mwaka huu kwa ligi kuu ya Uingereza (EPL) pekee. 

 “Inawezekana nikafanya usajili wa mchezaji mmoja na akawa ni huyo pekee, nilitoa listi ya wachezaji watano ninaowahitaji kwa klabu yangu na nasubiri kuona kama itawezekana“. Amesema Mourinho. 

Kocha huyo pia ameonesha kutofurahishwa na matokeo ya timu yake katika michezo ya kirafiki iliyocheza mpaka sasa, huku akilaumu kutokuwepo kwa wachezaji wake tegemeo ambao bado wapo likizo tangu michuano ya kombe la dunia ilipomalizika. 

Man United imefanya usajili wa wachezaji watatu pekee mpaka sasa ambao ni , Diogo Dalot kutoka Fc Porto, Fred aliyesajiliwa kutokea Shaktar na mlinda mlango Lee Grant. 

Hatua hiyo imekuja baada ya Man United kupokea kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Liverpool usiku wa jana katika mfululizo wa michezo ya kirafiki ya, International Club Championship (ICC) inayoendelea barani Asia na Marekani. 

Matokeo ya michezo mingine ya kirafiki iliyochezwa usiku wa jana ni pamoja na Manchester City kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Bayern Munich, Barcelona ikiifunga Tottenham Hortspur kwa mikwaju ya penalti 5-3, Chelsea ikiifunga Inter Milan kwa penalti 5-4 huku Juventus ikishinda kwa penalti 4-2 dhidi ya Benfica.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad