Watu wanne wakiwamo wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manane ya uhujumu uchumi ikiwamo kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba katika vyeti vya tathmini ya uharibifu wa mazingira.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga aliwataja washtakiwa hao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde kuwa ni Ofisa wa Mazingira NEMC, Deusdith Bulamire (38), Sekretari, Edna Lutanjuka (51) na mkulima Mwaruka Mwaruka (42).
Mwingine ni Mkaguzi kutoka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG), Dawson Barwongeza.
Akisoma mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao, wakili Katuga alidai washtakiwa hao kwa pamoja kati ya Machi 28, 2017 na Novemba 4, 2017 wakiwa Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kughushi Vyeti vya Tathmini ya Uharibifu wa Mazingira (EIA).
Washtakiwa Bulamire, Lutanjuka na Mwarukwa wanadaiwa kuwa Oktoba 10, 2017 walighushi saini ya Waziri Makamba kwenye cheti cha EIA wakijaribu kuonesha sahihi hiyo ni ya waziri huyo wakati si kweli.
Kwa pamoja washtakiwa hao wote wanadaiwa kuwa kati ya Machi 28 na Novemba 4, mwaka jana walijipatia Sh30 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa F1195 CPL Yohana Mtweve kwa madai kuwa wangeweza kufanya tathmini ya uharibifu wa mazingira na kumpatia cheti ambacho kinatolewa na NEMC kitendo ambacho si kweli.
Pia, wanadaiwa kuisababishia hasara ya Sh20 milioni NEMC.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza wala kutoa dhamana kwenye kesi hiyo.
Washtakiwa wamepelekwa rumande na kesi iliahirishwa hadi Julai 18, 2018 kwa ajili ya kutajwa.