Wakala wa Samatta athibitisha safari ya La Liga
0
July 28, 2018
NA ELBOGAST MYALUKO
Nyota wa Tanzania anayekipiga katika klabu ya soka ya KRC Genk ya ligi kuu ya Ubelgiji Mbwana Samatta, huenda akatua kwenye ligi kuu ya soka ya Hispania kwa msimu ujao, baada ya klabu ya Levante kuonesha nia ya kuhitaji huduma yake.
Wakala wa Samatta Jamal Kasongo ameweka wazi hilo kupitia East Africa Television ambapo ameeleza kuwa tayari klabu hiyo imeshatuma ofa kwa klabu ya Genk ikimhitaji Samatta ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania.
''Ni kweli pande zote mbili zipo kwenye mazungumzo kinachoonekana kuchelewesha usajili huo ni gharama ambayo Genk wanahitaji na kiasi walichotoa Levante ambacho ni Euro milioni 4 zaidi ya shilingi bilioni 10 huku Genk wakihitaji Euro milioni 10 zaidi ya shilingi bilioni 26'' - amesema.
Kasongo ameongeza kuwa kuna ofa pia kutoka klabu ya CSKA Moscow ya Urusi lakini hawajaipa nafasi sana kutokana na ndoto ya Samatta ni kukipiga katika Ligi Kuu ya England, ambayo ndio chaguo lake namba moja na La Liga kama namba mbili hivyo yupo tayari kujiunga na Levante.
Akiwa na Genk ambayo alijiunga nayo mwaka 2016, akitokea TP Mazembe ya DRC, Samatta amecheza mechi 66 na amefanikiwa kufunga mabao 19. Tayari Samatta ameshacheza michuano ya Europa League msimu uliopita lakini timu yake ilishia hatua za awali.
Tags