Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imemkamata raia wa Marekani, Loniel Royford (63) kwa tuhuma za dawa za kulevya kilo 2.18 aina ya heroin.
Kamishna wa operesheni, Frederick Milanzi amesema Royford alifika Juni 29 akijitambulisha kama mtalii lakini alitiliwa shaka wakati anaondoka nchini Julai 4. “Tulimtilia shaka, mtalii amekuja na kukaa siku chache, yaani Juni 29 na akataka kuondoka Julai 4, tukampekua akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA),” alisema Milanzi.
Milanzi alisema licha ya mashine za X-Ray kukagua bila kuona dawa sehemu hizo mwilini na kwenye mizigo yake, polisi hawakumruhusu kuondoka.
“Hawa watu wanatumia mbinu za hali ya juu, baada ya kumkagua kwa kina tulibaini amefumua begi na kuweka kitambaa kingine maalumu ambacho si rahisi x-ray kubaini kama kuna dawa za kulevya,” alisema.
Alisema hata walipopekua mabegi yake na kutoa mizigo yote lakini hawakuona dawa na kwamba baada ya kufumua begi hilo, walikuta kilo 2.18 za dawa aina ya heroin.
“Tulizipeleka kwa mkemia mkuu wa Serikali na akathibitisha ni heroin,” alisema. Pamoja na huyu, raia wengine wawili wa Marekani, wenye asili ya India mtu na mkewe, walikamatwa Juni 28 wakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kwa tuhuma za kukutwa na kilo 8.9 za heroin.
Milanzi aliwataja raia hao kuwa ni Imtiaz Hussein Sheikh (53) na mke wake, Miranda Sheikh (61).
“Taarifa zilitoka hapa kwetu makao makuu lakini tulituma ofisa wetu ambaye alikwenda Kia na akashirikiana na polisi wa kule hadi kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao,” alisema.