Watu sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kituo cha Sirari wilayani hapa Mkoa wa Mara kwa tuhuma za kula njama ya kuanzisha mapigano baina ya koo mbili za Wakira na Wanyabasi katika vijiji vya Kebweye na Kyoruba.
Akizungumza leo Jumatatu Julai 16, 2018 Kamanda wa polisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amesema watu hao walikamatwa kwa tuhuma za uchochezi wa koo wakigombea mipaka ya vijiji hivyo.
Amesema walipanga kuanzisha vurugu lakini polisi walipata taarifa na kufanikiwa kuizima.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kebweye, Marwa Nyasoko amesema vurugu hizo ziliibuka Julai 13, 2018 baada ya wananchi wa kijiji cha Kyoruba kuvamia miji iliyopo mpakani na kuchoma nyumba moto.
"Saa tatu usiku walivamia miji mitatu ya mpakani wakachoma nyumba mbili za nyasi na kukatakata bati zilizokuwa zimeezeka nyumba moja lakini polisi wakawa wamefika na kuwatawanya,” amesema Nyasoko.