Watu Wamtolea Povu Lulu Kushindwa Kumzika Patrick

BAADA ya mazishi ya mtoto wa muigizaji Rose Alphonce ‘Muna’, Patrick kufanyika kisha rafiki yake kipenzi, muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ kushindwa kuhudhuria, siri ya mrembo huyo kutoonekana msibani imefichuka!

Marehemu Patrick alizikwa juzi kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar baada ya kuagwa katika Viwanja vya Leaders Club. Gumzo la Lulu kutoonekaa liliibuka kwenye Viwanja vya Leaders wakati watu walipoanza zoezi la kuaga huku mastaa karibu wote wakiwa wameshaaga na Lulu kutoonekana.

“Mh! Mbona sielewi, naangalia mastaa wote wanaaga lakini Lulu sijamuona hapa kulikoni? Ana shida gani huyu mtoto,” alisikika mmoja wa waombolezaji anayeonekana kuwa na jicho la kidaku.

Kama hiyo haitoshi, mdaku mwingine aliyekuwepo msibani hapo, alinaswa na kinasa sauti cha Ijumaa Wikienda akienda mbali zaidi kwa kusema haiwezekani Lulu akashindwa kumzika Patrick ambaye alikuwa kipenzi chake na ukizingatia ni rafiki mkubwa wa Muna.“Haiingii akilini, kuna kitu tu lazima. Yaani mastaa karibu wote waje hapa halafu yeye ashindwe kufika, ni kitu cha kushangaza sana kwani yeye ni mtu wa karibu sana na familia ya Muna.”

MAPAPARAZI WAJIRIDHISHA

Mara baada ya mapaparazi wetu kujiridhisha kwamba Lulu hajakanyaga msibani kuanzia pale nyumbani kwa baba wa marehemu, Peter Zakaria Mwananyamala- Kisiwani, Leaders na hata makaburini ndipo walipochimba na kunasa mambo kibao yaliyofichika.

Ijumaa Wikienda lilianza kuzungumza na watu wa karibu na familia ya Peter ambao waliweka wazi kuwa wamesikitishwa na kitendo cha Lulu kushindwa kufika msibani, achilia hata kutoa pole.

“Lulu tumemshangaa sana, kweli kabisa unashindwa kutoa hata pole? Yaani Peter huyu ambaye alijitoa kwa hali na mali wakati wa kesi yake ya kuua bila kukusudia kweli anashindwa hata kumpigia simu kumpa pole? “Lulu ni wa kushindwa hata kufika hapa kwenye mazishi kweli? Yeye ni nani haswa hata ashindwe hata kuona ubinadamu katika jambo kama hili?” alihoji mwanafamilia huyo wa Peter.

SIRI YAFICHUKA

Mmoja wa wasanii ambao walikuwa upande wa Peter ambaye pia alikuwa akisimamia mambo mbalimbali katika msiba huo aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini, alivujisha siku kuwa kilichomfanya Lulu ashindwe kuhudhuria ni aibu.

“Ni aibu tu maana kama ulivyojua yeye alikuwa upande ule wa Muna, alionekana siku ya kwanza akiwa anaratibu msiba na yeye ndiye miongoni mwa wasanii waliokuwa wanamuunga mkono Muna kukataa baba yake marehemu asimzike mwanaye hivyo aliona akijitokeza pale wapambe wanaweza hata kumzomea kwa jinsi hali ya hewa ilivyokuwa imechafuka,” alidai mtu huyo.

NI MAMBO YA KISHERIA?

Baadhi ya waombolezaji walikwenda mbele zaidi na kudai kuwa, yawezekana Lulu kutomzika Patrick kumetokana na masuala ya kisheria kwamba haruhusiwi kwenda kwenye mijumuiko ya watu kama vile msibani, harusini na kwingineko lakini mmoja wa wanasheria alisema Lulu anaweza kwenda popote hata kuolewa anaruhusiwa.

PETER AFUNGUKA

Katika mahojiano maalum na Ijumaa Wikienda, baba wa marehemu Patrick alieleza kuwa amesikitishwa na kitendo cha Lulu kushindwa kumpa pole kwa msiba huo mzito wakati alijitoa kwa hali na mali kumsaidia alipopata matatizo ya kimahakama. Alisema, wakati Lulu alipokuwa akikabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia muigizaji Steven Kanumba, alipokuwa mahabusu kabla ya kuhukumiwa, alimsaidia sana.

“Nilimsaidia sana kwa kumtumia pikipiki iliyokuwa inabeba chakula kila siku kwa muda mrefu, nilitoa hadi gari langu kwa ajili ya kumpeleka mahakamani lakini leo hii nashangaa sana anashindwa, hata kunipa pole?” alihoji Peter kwa uchungu.

MAMIA WAMUAGA

Katika safari yake ya mwisho Patrick ambaye alikuwa kipenzi cha watu wengi mtandaoni kutokana na muonekano wake, mamia ya watu walijitokeza kumuaga wakiwemo wasanii mbalimbali. Wakati Peter alipokuwa akitoa neno la shukurani, aliwataka watu waliokuwa wanamsema vibaya mitandaoni kuhusu yeye na Muna waache maana ni mke wake halali.

Alisema, alimtolea mahari na mama yake Muna akamkabidhi hivyo asingependa kuona suala hilo linajadiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii. Lakini wakati akiyasema hayo, Muna alionekana kutikisa kichwa kuashiria kutokubaliana naye pamoja na kwamba walikuwa wameshapatanishwa, kitendo kilichozua minong’ono kwa watu waliokuwa karibu na mapaparazi wetu.

Kwa upande wake muigizaji Wema Sepetu alipopewa kipaza sauti, alisema anaelewa maumivu anayopitia Muna na kwamba anamuombea kwa Mungu aweze kusimama imara. Mrembo huyo ambaye aliwahi kuwa shosti wa karibu na Muna kisha kugombana, alitumia fursa hiyo kumaliza tofauti zake na kusema yaliyopita si ndwele, wagange yajayo.


Kwenye tukio hilo, baadhi ya wanaume ambao walitajwa kutembea na Muna kwa nyakati tofauti kama Casto Dickson na Joel Luaga ambaye ndiye anatajwa kuwa na uhusiano na Muna kwa sasa, walishindwa kuhudhuria mazishi hayo.

Wasanii waliojitokeza kumuaga katika Viwanja vya Leaders juzi licha ya Wema Sepetu ni Steven Mengere ‘Steve Nyerere’, Khadija Shaban ‘Keisha’, Halima Yahya ‘Davina’, Emmanuel Mgaya ‘Masanja’, Jimmy Mafufu, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ na wengine wengi.

TUJIKUMBUSHE

Patrick alipatwa na umauti Julai 3, mwaka huu nchini Kenya baada ya kuugua na kulazwa kwa takriban siku sita. Mara baada ya kufariki dunia, uliibuka mvutano mkali kati ya Muna na mumewe juu ya suala zima la nani baba halali wa mtoto huyo. Peter alisema yeye ni baba halali kwani alimuoa Muna kwa ndoa takatifu na mtoto ni wake licha ya kumuoa akiwa na ujauzito wa miezi mitatu.

Baada ya kuyasema hayo, Muna aligeuza upepo kwa kusema baba wa mtoto ni Casto na kwamba shughuli za msiba zitafanyika nyumbani kwake Mbezi na si kwa mumewe huyo, Mwananyamala- Kisiwani. Kutokana na mvutano huo, Steve Nyerere alilazimika kuingilia kati na kutokana na busara zake alifanikiwa kuweka mambo sawa kwa kuzungumza na wanandoa hao ambapo Muna aliridhia msiba kufanyika nyumbani kwa mumewe.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad