Watu Wanaopeana Talaka, Wanaongoza Kwa Kuwa na Maambukizi Mapya ya Ukimwi

TUME ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), imesema watu wanaopeana talaka, wanaongoza kwa kuwa na maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi kwa asilimia 11.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Tanga, Juma Bilingi, alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo   vya habari  Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, jana.

Bilingi alikuwa akitoa matokeo ya utafiti wa viashiria na matokeo ya ugonjwa huo kwa mwaka 2016/17.

Alisema maambukizi kwa watu walioko katika ndoa yamefikia asilimia 4.8.

“Pia kuna kundi la waliooa na kuolewa ambao kiwango chao cha maambukizi mapya ni asilimia 1.8, wajane ni asilimia 13, waliotengana ni asilimia 11.

“Kwa hiyo utafiti huu umetupatia picha halisi ya maambukizi mapya katika makundi mbalimbali,” alisema Bilingi.

Kwa mujibu wa Bilingi, utafiti huo ambao ni wa nne kufanyika, maambukizi mapya yanaonyesha Watanzania 81,000 wanapata virusi vya ugonjwa huo  kila mwaka ambayo ni   asilimia 9.2.

“Utafiti wetu umebaini kwa mwaka Watanzania kiasi nilichokitaja hapo juu wanapata maambukizi mapya, lakini tunaendelea na juhudi za kila aina   kupambana na hali hiyo.

“Katika utafiti huo uliofanyika kati ya mwaka 2016 na 2017, mwitikio wa Watanzania waliokusudiwa kupimwa walijitokeza kwa asilimia 94  huku kaya zilizochaguliwa zikiwa ni 16,198.

“Kaya zilizopatikana zilikuwa ni 15,564, wakati zilizohojiwa zilikuwa ni 14,811. Katika eneo hili kulikuwa na changamoto kiasi kwa sababu zipo kaya ambazo ziligoma kuhojiwa,”alisema.

Alisema utafiti huo  ulifanyika katika maeneo ya VVU, maambukizi mapya, kufubazwa kwa virusi na homa ya ini.

Utafiti huu mpya umekuja ikiwa ni miaka minne tangu ulipofanyika utafiti mwingine kati ya mwaka 2011 na 2012 ambao kwa kiwango fulani umeonyesha matokeo yanayotofautiana au kufanana katika baadhi ya maeneo.

Alisema maambukizi ya VVU  kwa watu wenye umri wa miaka kuanzia 15 hadi 49 yamefikia asilimia 4.7.

Katika eneo hilo, alisema wanawake waliopata virusi ni asilimia 6.2, wakati wanaume ni asilimia 3.1 na watoto wenye umri wa kuanzia miaka 0 hadi 14 ni asilimia 0.4.

“Mgawanyo wa utaalamu  unaonyesha katika kundi hili, watoto wa kike ambao ni   asilimia 0.5 na wa kiume asilimia 0.3, wamekutwa na VVU,” alisema.

WATU WAZIMA

Alisema watu wazima kuanzia umri wa miaka 50 na kuendelea  maambukizi yao yamefikia asimilia 5.8 na katika mgawanyo  wanawake ni asimilia 6.5, wakati wanaume ni asilimia tano.

“Takwimu hizi zote zinazochukuliwa zimekubaliwa na kukidhi vigezo vya  mataifa ambavyo vimekuwa vikitumika duniani,”alisema.

Alisema  maambukizi mapya katika maeneo ya mijini kwa watu wenye umri kati ya   miaka 15 hadi 49     yamefikia asilimia 7.8.

VIJIJINI

Alisema katika umri huo, maeneo ya vijijini yamekutwa na maambukizi mapya ya asilimia 4.2, wakati wanawake waliopo kwenye maambukizi hayo ni asilimia 5.1 na wanaume ni asilimia 3.2.

“Kwa kweli kundi hili linapaswa kumulikwa zaidi na zaidi kwa sababu kiwango hiki ni kikubwa ingawa katika kundi hili utaona wasichana asilimia 80 wanapaswa kumulikwa pia.

Aliitaja mikoa miwili yenye maambukizi ya juu kuwa ni Iringa yenye maambukizi asilimia 11.3 na Njombe yenye asilimia 11.4.

Aliitaja mikoa yenye maambukizi kidogo kuwa ni Lindi yenye asilimia 0.3 na Arusha yenye asilimia 1.9.

Mtanzania
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad