Waziri Awapiga Marufuku Wanaume Kutoa Talaka kwa Simu

Waziri Awapiga Marufuku Wanaume Kutoa Talaka kwa Simu
Waziri  wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Moudline Castico, amekemea tabia ya baadhi ya wanaume kuwataliki wake zao kupitia ujumbe wa simu.

Akizungumza na wanachama wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) katika Tawi la Kiembesamaki Unguja, Waziri Castico alisema kitendo cha kutaliki mke kwa ujumbe wa simu (SMS) ni dharau na udhalilishaji.

Waziri huyo alieleza masikitiko yake kwamba baadhi ya wanaume wanaofanya hivyo ni wale waliowezeshwa na wake zao wanaojituma, ambapo hali za waume hao zilikuwa duni wakati wakioana.

Alisema wapo wanaume wanaosaidiwa kujenga nyumba na hata kununuliwa magari na wake zao, lakini hatimaye wanawatoa thamani na kuwanyanyasa baada ya kupata wanawake wanaowaona ni wazuri zaidi.

Alieleza kuwa jambo baya zaidi ni kuacha kuwashughulikia watoto kwa kuwanyima huduma na matunzo hali inayowasukuma kuzurura mitaani na kuingia katika ajira mbaya na kusababisha wafanyiwe vitendo vya udhalilishaji.

“Dini zote zinaitambua ndoa kuwa ni kitu cha heshima na ina maadili yanayopaswa kufuatwa na watu wanaoamua kushirikiana kimaisha.

“Hata hivyo, iwapo kunatokezea sababu ya wanandoa kutengana, lazima waachane kwa wema, heshima na mafahamiano ili ihsani waliyokuwa nayo wakati wakiwa pamoja iendelee na hasa wanapokuwa wamejaaliwa kupata watoto.

“Kuacha kuna taratibu zake, akina baba mnapowapenda wake zenu muwe na busara, mnapoanza pamoja lazima muende pamoja kama unavyombembeleza siku ya kwanza.

“Sio kashakuchumia mali zako, ushakuwa na uwezo, kakununulia kigari unampelekea talaka kwenye simu,” alisisitiza waziri Castico.

Katika hotuba hiyo pia Castico aliwanasihi wanawake kuwa waaminifu kwenye ndoa zao hata pale waume zao wanapokengeuka, badala ya kutaka kulipa kisasi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad