Jafo ametoa maagizo hayo alipofanya ziara katika shule hiyo, na kusema wazi kuwa hajafurahishwa na usimamizi uliopo katika shule hiyo.
Alisema shule hiyo imekuwa ya 453, na imeleta picha mbaya kwa jamii kwa kuwa ni shule yenye sifa maalumu, upako maalumu na tunu kwa nchi.
“Hii ni fedheha ambayo haijawahi kutokea. Shule iliyokuwa na sifa kitaifa leo imekuwa dhaifu. Ninyi mna unyafuzi wa kitaaluma shuleni kwenu. Hali yenu ni mbaya sana. Ni miongoni mwa shule chache zenye walimu 87 ambao ni wengi. Kibaha ina walimu 52 tu lakini inakuwa ya kwanza. Kuna kitu ambacho si sawa.
“Tangu juzi nilisema nitakuja. Nimekuja kuwaambia kuwa hamjanifurahisha hata kidogo kwa Shule ya Jangwani kuwa na matokeo mabovu kama haya. Inawezekana mkawa na sababu nyingi sana za kujieleza lakini hazina ushahidi wa moja kwa moja,” alisema.
Jafo alisema wanafunzi wamewataja kwa majina walimu ambao hawafundishi shuleni hapo, na kwamba upo uwezekano mkubwa wanakwenda shule za binafsi kufundisha, wengine wanawapa watoto hao kujiandikia notisi, na mada za masomo hawazimalizi.
Alimweleza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema kuwa shule hiyo imemtia aibu, hivyo anataka watu wawajibike katika maeneo yao.
“Sijafurahishwa na usimamizi wa shule hii. Mpaka kesho (leo) nataka mfanye mabadiliko ya uongozi Sekondari ya Jangwani. Pia fanyeni mabadiliko ya walimu. Wale wote waliokaa muda mrefu muwabadilishe na hapa mlete walimu wengine.
“Haiwezekani mwalimu moja anakaa muda mrefu. Badilisheni walimu wa Jangwani. Leteni wengine waje walete mabadiliko Jangwani. Mpaka Jumatatu nataka nilete mabadiliko hayo ofisini kwangu,” alisema.
Alisema anaamini walimu waliokaa zaidi ya miaka mitano watabadilishwa, kwani wasipobadilishwa hata wakiletwa wapya hawatafanya vizuri kwa sababu kuna wahenga wanaoijua Jangwani. “Ukijiridhisha mwalimu anafanya vizuri nani tegemeo kubwa mmbakishe Jangwani asiondolewe. Wengine wote waondolewe haraka. Rais nenda kafanye mabadiliko ya haki,” alisema.
Waziri huyo alisema anataka shule hiyo mwakani isomwe katika takwimu nyingine nzuri, kwani anataka vijana warudishe thamani yao kwani hivi sasa imeshuka.
Waziri Jafo aliwataka walimu waliobaki kufanya kazi kwa bidii, na wale wote wanaofanya kazi katika shule binafsi wabainishwe, kwa kuwa wanataka kuona mabadiliko katika shule hiyo.
Pia aliwaeleza wanafunzi wako pale kwa ajili ya kusoma si kwa sketi za rangi ya chungwa, hivyo wasome na kuacha kutumia simu za WhatsApp kwa ajili ya kuangalia picha mbaya, ama kuangalia ni namna gani watakuwa warembo.
Aliongeza kuwa wanafunzi wengi shuleni hapo wanajihusisha na masuala ya uasherati, hivyo kama matendo yao yapo hivyo elimu haiwezi kuwa rafiki yao.
“Suala la uasherati hata wakubwa linawashurutisha je ninyi mtaweza vipi kulibeba? Tabia ya kujihusisha na mambo yasiyowahusu ishindwe na kulegea. Kwani watoto wa Jangwani mmekuwa mabingwa wa kujadili mambo mengine na si masomo,” alisema.
Alisema kuna changamoto ameambiwa zikiwemo za mabweni shuleni hapo, watazifanyia kazi kuhakikisha vijana hao wanapata utulivu mzuri.
Aliwataka wanafunzi waliobaki kuhakikisha wanajitathmini ili kuondoa aibu hiyo kwa taifa. Jafo alisema, kuna mlizi mmoja mtu mzima anawarubuni wanafunzi hao, hivyo mpaka ikifika leo awe ameshaondolewa.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Palela Msongela alisema, shule hiyo imeshika nafasi ya 451 kati ya 453 kitaifa.
Alisema shule hiyo ilianza kuonesha matokeo ya ufaulu duni kutokana na matokeo yasiyoridhisha kwenye mtihani wa Moko Mkoa uliofanyika Februari, mwaka huu, ambapo ilikuwa katika kundi la shle 10 za mwisho kimkoa.
Alisema baada ya matokeo hayo Idara ya Elimu Sekondari ilifanya ufuatiliaji wa kitaaluma mara tu baada ya matokeo ya Kidato cha Sita 2018, kwa kuongea na Mkuu wa Shule, walimu wa Kidato cha Sita, walimu wote na wanafunzi wa Kidato cha Sita 2018 na kutoa ushauri.
Alikiri kuwa uongozi wa shule haukufanyia kazi ushauri uliotolewa na maofisa katika ufuatiliaji uliofanyika Februari mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kudhibiti utoro.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Geradine Mwanisenga alisema karibu asilimia kubwa ya watoto wenye udhaifu wanapelekwa shuleni hapo, na wa mikoani kwa kuwa wapo karibu na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema hao wa mikoani wanapofika wanapelekwa kwenye hosteli zisizo na maadili bila wazazi wao kuomba ushauri.
“Kati ya watoto 20 waliofeli wanane wapo hosteli za nje. Sita wadhaifu,” alisema.
Aliongeza kuwa, changamoto ipo kwa Kidato cha Tano na Sita, kwani taaluma ya A level sio nzuri, na kushauri waangalie utendaji kwa shule nzima kwani O level imekuwa na matokeo mazuri.