Waziri Mbarawa: Sitamvulimia Mtu Yeyote


Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa amesema katika uongozi wake ndani ya wizara hiyo hatowavumilia watendaji wanaoshindwa kusimamia kwa ufanisi miradi ya maji.


Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 19, 2018 wakati akifungua kongamano la kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya sekta ya maji nchini.


Mbarawa amesema amebaini kuna watu wamepewa dhamana ya kusimamia miradi lakini wanashindwa kufanya kazi hiyo kama inavyotakiwa.


Amesema katika muda mfupi alioingia kwenye wizara hiyo amekutana na miradi mingi ambayo imeshindwa kukamilika ndani ya muda uliopangwa kutokana na uzembe.


"Miradi mingi ya maji ni ya muda mrefu, tatizo sio pesa kuna uzembe unafanyika huenda ni kwa maslahi binafsi. Maeneo mengine mkandarasi yupo eneo la mradi lakini kazi imesimama,"amesema.


"Hili ni tatizo hatuwezi kwenda hivi  lazima tubadilike kama  wizara, hatuwezi kumpa kazi mkandarasi kwa sababu tunamfahamu au anazunguka koridoni. Tutawapa kazi wakandarasi wenye uwezo na viwango na tutawasimamia wafanye kazi kwa ubora unaostahili.”


Profesa Mbarawa pia amewataka wakandarasi watakaopewa kazi za miradi ya maji kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa uaminifu bila kujali utaifa wao.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, mhandisi Stella Manyanya amesema kongamano hilo  ni muhimu kwa kuwa  linatoa fursa kwa sekta binafsi na Serikali kushirikiana katika kuhakikisha maji yanapatikana kwa urahisi.


Amesema kupitia kongamano hilo, Serikali na sekta binafsi watakuwa na  mwelekeo mmoja wa kuleta matokeo makubwa katika sekta ya maji na viwanda.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad