WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Balozi wa Tanzania nchini China, Balozi Mbelwa Kairuki na amempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya tangu aende huko.
Amekutana na Balozi Kairuki jana katika makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam, na amemtaka Balozi huyo ahakikishe anaboresha mahusiano kati ya Tanzania na China.
“Ni lazima nikupongeze kwa namna unavyoendelea kufanya kazi na unavyojitahidi kudumisha mahusiano na China. Tunashukuru kwamba wageni wanaokuja hapa nchini kutoka China wanatoa taarifa nzuri na jinsi unavyosaidia kuitangaza nchi yetu huko nje.”
“Umefanya kazi nzuri ya kuwaelekeza wawekezaji wa huko kwamba wakati tunaunda Serikali na kutengeneza mfumo wa utawala, tuliamua kujenga kwanza mifumo imara na kutambua fursa zetu tulizonazo ili baadaye Watanzania waweze kunufaika na hizo fursa.”
Amesema kupitia utaratibu huo, Serikali ilitaka Watanzania wamiliki ardhi ndipo mgeni apate, na kama kuna uzalishaji wowote unafanyika basi Mtanzania awe wa kwanza kunufaika, Serikali inufaike na mwekezaji naye anufaike.
“Tunakushukuru kwamba umesaidia kuwaambia wachina watulie wakati Serikali ikirekebisha mifumo yake. Na wao wameyaona mabadiliko hayo, kwani tumesimamia vita dhidi ya rushwa, na wao walikuwa ni waathirika wakubwa, lakini pia tumeongeza uwajibikaji. Watu wetu sasa wanawajibika kwenye viwanda na makampuni yao na Watanzania kwa ujumla, wametambua umuhimu wa kufanya kazi ili waweze kuishi,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Serikali hivi sasa iko kwenye programu ya kutangaza utalii uliopo nchini hasa kwa kuamua kuagiza ndege kubwa zitakazobeba watalii na kuwaleta moja kwa moja hapa nchini.
“Sasa hivi tumepata wageni maarufu kutoka nje ya nchi akiwemo Rais mstaafu wa Marekani, Mheshimiwa Barack Obama na wachezaji maarufu duniani, kwa hiyo tunaendelea na mikakati yetu ya kutangaza utalii huko nje.”