WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini wasibaki nyuma katika suala zima la kuwekeza kwenye viwanda ili waweze kuendana na azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Serikali ya awamu ya tano imeazimia kukuza uchumi wa viwanda. Nawaomba msiwe nyuma katika suala hili, tumieni fursa ya ardhi tuliyonayo hasa katika ujenzi wa viwanda vya usindikaji ili kuongeza thamani ya mazao,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa rai hiyo leo (Alhamisi, Julai 12, 2018) wakati akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 52 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT). Mkutano huo wa siku mbili, umehudhuriwa na maaskofu zaidi ya 80, wenyeviti wa makanisa na wawakilishi wa vyama vishiriki.
Amesema uwepo wa viwanda hivyo utachangia ukuaji wa sekta ya kilimo na kuongeza ukuaji wa mnyonyoro wa thamani ya mazao. Akitoa mfano fursa zilizopo hivi sasa, Waziri Mkuu aliwaeleza Maaskofu hao kwamba bei ya ufuta kwa mwaka huu imepanda na kufikia sh. 3,100/- ikilinganishwa na sh. 1,400/- ambayo ilikuwa ni bei ya mwaka jana.
Ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa dini kwa kwa kubwa wanayofanya ya kukemea maovu kama vile ujangili, ukatili wa kijinsia na matumizi ya dawa za kulevya.
“Serikali inaheshimu mahubiri yenu sababu tunajua yana nguvu sana. Kupitia mahubiri yenu, watu wakimjua Mungu, watakuwa na hofu ya Mungu, kwa hiyo watu watakuwa waadilifu na maovu mengine yatapungua,” amesema.
“Nitumie fursa hii kuwajulisha kwamba Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa wa nchi zilizosimamia vizuri mapambano dhidi ya dawa za kulevya barani Afrika. Kwa hiyo tumepewa heshima ya kuandaa mkutano mkubwa wa kimataifa utakaofanyika hapa nchini Septemba, mwaka huu.”
Amesema mshikamano uliopo baina ya viongozi wa Serikali na viongozi wa dini hauna budi kuendelea. “Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wajenge mshikamano wa pamoja na viongozi wa dini katika maeneo yao husika. Viongozi wa Kitaifa nasi, tutaunga mkono katika ngazi ya kitaifa,” amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na maaskofu hao, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania, Askofu Dkt. Anilikisa Cheyo alisema Jumuiya hiyo inaendelea kusisitiza suala la umoja na mshikamano wa Kitaifa.
“Suala la umoja wa kitaifa na amani ya nchi yetu ni masuala mtambuka; tena ni nguzo ya utaifa wetu. Tunashukuru jinsi Serikali inavyosimamia masuala haya kwa hekima na uthabiti. Tunaahidi kuwa tutaendelea kuliombea Taifa letu pamoja na viongozi wake ili mzidi kuilinda amani ya Taifa letu pamoja na watu wake.”
“Hata wakati inapotokea masuala haya yanapoguswa au kuumizwa, Kanisa limeendelea kuhimiza mara zote kutafuta ufumbuzi wake kwa njia ya mazungumzo,” amesema.