Mahakama nchini Pakistani imemhukumu aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Nawaz Sharif kifungo cha miaka 10 gerezani kwa makosa ufisadi unaohusu majengo manne ya kifahari jijini London.
Nawaz Sharif,ambaye kwa sasa yuko London alihukumiwa akiwa hayuko mahakamani, na mwenyewe alisema kuwa hukumu hiyo ina mlengo wa kisiasa.
Jaji Mohammad Bashir amemtaka Sharif kutumikia kifungo cha miaka 10 kwa kosa la kumiliki mali yenye gharama kubwa kuliko kipato chake na mwaka mmoja kwa kutotoa ushirikiano na mamlaka inayopambana na vitendo vya rushwa, NAB.
Binti yake, Maryam Nawazi Sharif amehukumiwa kifungo cha miaka saba kwa kushirikiana na babaye kwenye uhalifu huo na mwaka mmoja kwa kutotoa ushirikiano kwa mamlaka za kiuchunguzi huku mkwewe Nawaz akihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja kwa kutotoa ushirikiano.
Sharif na Maryam wametozwa faini ya pauni milioni 8 na pauni milioni mbili.Kwa sasa wote wako jijini London ambapo mke wa Sharif, Kulsoom Nawaz anapata matibabu kutokana na maradhi ya saratani.
Panama Papers zilizovuja mwaka 2015 zilitoa taarifa kuwa watoto kadhaa wa Sharif walikuwa na mahusiano na makampuni yaliyo nje, ambayo yalidaiwa kupitisha fedha kwa ajili ya kununua mali nje ikiwemo majengo ya anasa jijini London
Familia yake, hatahivyo, inasisitiza kuwa wanamilimiliki mali hizo kihalali. Katika sehemu ya hukumu, Mahakama imetaka mali hizo zitaifishwe kwa serikali.
Waandishi wa habari nchini Pakistani walikita kambi nje ya makazi ya Avenfield, ambako familia ilikuwa ikitazama kesi.