Wema Sepetu Amekaa Jirani Sana na Jela!


WEMA Sepetu alihukumiwa Ijumaa, ama kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini. Alikutwa na hatia ya kumiliki na kutumia dawa za kulevya.

Hukumu aliyopewa Wema yenye kumpa chaguo la kulipa faini ni nafuu kubwa kwake na hutakosea ukisema ni upendeleo mkubwa. Watu wengi wanakutwa na hatia ya mara moja wananyimwa kulipa faini na kuamriwa kwenda jela, ila yeye si mara ya kwanza bado kapewa fursa ya kulipa faini iliyo ndani ya uwezo wake.

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi 'Sugu', aliachiwa kutoka jela Mei mwaka huu, alipokuwa akitumikia kifungo cha miezi mitano. Sugu alikutwa na hatia ya kuzungumza maneno yenye kumfedhehesha Rais. Katika hukumu yake hakupewa chaguo la faini ingawa lilikuwa kosa la kwanza.

Mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali, Januari mwaka jana alikutwa na hatia ya kufanya vurugu kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, wakati wa uchaguzi wa baraza la madiwani. Lijualikali alihukumiwa kwenda jela miezi sita bila faini. Hata hivyo, Lijualikali alishinda rufaa yake Mahakama Kuu.

Julai 23, 2008, fundi wa Bongo Fleva, Khalid Mohammed 'TID', alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela, kwa kosa la kumjeruhi mtu katika ugomvi wa klabu akiwa amelewa. TID hakupewa fursa ya kulipa faini japokuwa lilikuwa kosa lake la kwanza.

Wema aliwahi kufikishwa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, kesi ikiwa kugombana na kuharibu gari la aliyekuwa boyfriend wake, staa wa Bongo Movie, marehemu Steven Kanumba. Hata hivyo, kesi iliisha baada Kanumba kuomba kutoendelea na kesi.

Juni 9, 2011, Wema alihukumiwa kwenye Mahakama ya Mwanzo, Kinondoni, kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini Sh40,000 kwa kosa la kumtusi mwanamuziki na prodyuza wa Sharobaro Records, Raheem Nanji 'Bob Junior'. Wema alilipa faini.

Hivyo, Wema ni mzoefu wa matukio ya jinai, ila ana bahati, kwani hajapewa adhabu ya jela moja kwa moja kama wengine wengi. Hakimu wa juzi (Ijumaa) angeamua kuzingatia rekodi zake za nyuma, angeweza kumnyima fursa ya rufaa. Ni ushauri kwake kujichunga. Tayari ana rekodi chafu na siku nyingine si rahisi kupewa dirisha la rufaa. Atatupwa jela. Si kila siku ni Ijumaa.

Ndimi Luqman Maloto

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad