Klabu ya Yanga ambayo inatarajia kucheza mchezo wa kombe la shirikisho dhidi ya Gor Mahia Jumatano hii, imegomea usafiri walioandaliwa pamoja na hoteli mara baada ya kutua nchini humo.
Taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo iliandaliwa usafiri wa basi kutoka uwanjani hadi hotelini lakini ikaukataa na badala yake ikakodi usafiri wao na walipofika hotelini waligoma kuingia ndani ya hoteli bila kutoa sababu yoyote kulingana na maelezo ya katibu wa Gor Mahia, Ben Omondi.
“Tabia hii imekuwa ni kawaida kwa klabu za Afrika lakini nataka kuwahakikishia Yanga kuwa sisi hatujawahi na hatutoshiriki katika masuala ya kishirikina hata mara moja", amesema Omondi.
Juhudi za kumtafuta afisa habari wa klabu ya Yanga, Dismas Ten kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa kwani simu yake haikupokelewa mara kadhaa.
Katika michuano ya CECAFA Kagame Cup, Gor Mahia nao waligomea chumba cha kubadilishia nguo ambacho waliandaliwa kabla ya mchezo wa nusu fainali dhidi ya Azam Fc na badala yake walitumia korido kubadilisha nguo huku wakiituhumu Azam Fc kupuliza dawa katika chumba hicho.
Yanga na Gor Mahia zitachuana katika mchezo wa kundi D wa kombe la shirikisho, ambapo Yanga ikishika mkia katika kundi hilo mbele ya kinara USM Alger ya Algeria na Gor Mahia inayokamata nafasi ya pili.