Hiyo, ikiwa ni siku moja tangu wachezaji hao wafanye kikao kizito na Tarimba ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Kampuni ya Sportpesa Tanzania aliyebeba jukumu la kuhakikisha anakamilisha usajili wa mabeki hao.
Wachezaji hao hivi karibuni walijiondoa kwenye kikosi cha timu hiyo kilichosafiri kwenda Nairobi, Kenya kucheza na Gor Mahia katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa juzi Jumatano na Yanga kufungwa mabao 4-0.
Achana na kusambaa kwa picha zao wakidaiwa kutoka kwa kigogo huyo, habari kamili kutoka kwa chanzo cha uhakika ni kuwa katika kikao hicho Yondani alitaka dau la shilingi milioni 90 ambalo lilishuka na kufikia Sh milioni 70 huku akiomba mshahara wake wa kila mwezi uboreshwe kwa kipindi cha miaka miwili atakachosaini mkataba huo.
Mtoa taarifa huyo amesema, Yondani na Tarimba walifikia muafaka mzuri wa kusaini mkataba huo jana baada ya kupatiwa fedha zake za usajili kabla ya kujiunga na kikosi kilichorejea jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Gor Mahia utakaopigwa Julai 29, mwaka huu jijini Dar.
“Yapo baadhi ya mahitaji mengine aliyoyaomba na kutaka yawepo kwenye mkataba wake ambayo ni siri, wakati wowote kuanzia leo (jana) Alhamisi atasaini baada ya kufikia muafaka mzuri,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza:
“Baada ya Yondani kutoka ofisini kwa Tarimba, aliingia Kessy ambaye yeye alitumia dakika 45 kuzungumza na Tarimba na kikubwa aliomba ofa yake kabla ya kuzungumza zaidi.
“Kessy aliomba apatiwe shilingi milioni 60 ambazo bosi huyo akaomba apunguziwe hadi kufikia Sh milioni 40 ambazo Kessy alikataa na kusema kiasi hicho cha fedha ndiyo alichopewa msimu uliopita na kuomba apatiwe Sh milioni 50 ili asaini mkataba huo.
“Pia, Kessy aliomba aboreshewe mshahara wake anaouchukua kwa kila mwezi kutoka shilingi milioni mbili hadi kufikia tano huku akiomba apatiwe gari moja la kutembelea, ndiyo asaini mkataba huo.”
Taarifa ambazo zilifika mezani mwa gazeti hili ni kuwa Yanga wamekubali kumalizana na Yondani ambaye tayari ameshapewa kiasi cha fedha, huku Kessy akiwaambia wapo tayari kumpa Sh milioni 30 na gari, jambo ambalo beki huyo aliona siyo sawa, baada ya kujulishwa hivyo, ikabidi suala lake liwekwe pembeni kwa muda.
Alipotafutwa Tarimba kuzungumzia hilo, alisema: “Hakuna mazungumzo yoyote ya kiusajili niliyofanya kati yangu Kessy na Yondani na zaidi walifika ofisini kwangu kwa ajili ya kunitembelea.
“Mimi nitawezaje kusajili wakati sihusiki na masuala hayo ya usajili, wapo wanaohusika na usajili Yanga ni vema wakatafutwa.”
Alipotafutwa Kessy alisema: “Nipo kwenye mazungumzo mazuri na Yanga na kama mambo yakienda vizuri kwa maana ya kutimiza mahitaji yangu, basi nitasaini mkataba.”