Na Zitto Kabwe
KWA miaka mingi nimekuwa mtu ninayeamini katika kujipa muda wa upweke na kutazama dunia iliyonizunguka na kujiuliza maswali ama kunihusu mimi binafsi au kuhusu nchi yangu na Afrika.
Siku chache zilizopita, nilijipa muda huo wa utulivu kwa ajili ya tafakari. Swali kuu nililokuwa nikijiuliza ni hili; kwamba kama ningekuwa nimepewa mamlaka ya kuongoza Tanzania nini ningefanya tofauti na wanaoongoza sasa?
Hitimisho la tafakuri yangu likaangukia wilayani Ludewa mkoani Njombe. Kwenye utajiri ule wa chuma na mkaa wa mawe katika maeneo ya Liganga na Mchuchuma, nikaona kuna suluhisho la matatizo yetu yanayoendelea kiuchumi.
Mchuchuma na Liganga
Madini ya chuma na makaa ya mawe ndio msingi wa maendeleo ya viwanda duniani kote. Nchi yetu ina madini haya yote kwenye eneo moja, wilayani Ludewa mkoa wa Njombe.
Katika eneo la Mchuchuma kuna mashapo yenye tani bilioni 1.2 makaa ya mawe yenye uwezo wa kuzalisha Umeme 600MW kwa miaka 150. Makaa hayo pia hutumika kuyeyusha chuma na kuzalisha chuma cha pua. Vilevile eneo la Liganga lina mashapo ya madini ya chuma tani bilioni mbili ambayo ndani yake kuna madini yenye thamani kubwa ya Titanium na Vanadium.
Afrika nzima inajenga reli za kisasa na zote zinahitaji chuma kwa ajili ya kujenga njia za reli. Kenya na Ethiopia wamemaliza hatua za kwanza za reli zao ambapo Kenya imeshajenga kilometa 485 kutoka Mombasa mpaka Nairobi na Ethiopia kilometa 760 kutoka Addis Ababa mpaka Djibouti. Miradi yote hii mataruma ya reli yameagizwa kutoka nje na kuletwa Afrika na hivyo kuzalisha ajira huko kwenye nchi hizo (ambazo mataruma hayo yamezalishwa ).
Tanzania ingeamua, ingeweza kulisha miradi yote ya reli chuma kutoka Ludewa katika nchi za Kongo, Zambia, Angola, Uganda na Rwanda ambao wote wana miradi ya ujenzi wa reli na wamepanga kuagiza chuma kutoka China na kwingineko.
Bei ya tani moja ya chuma kwenye soko la dunia ni dola za Marekani 600 mpaka 1000. Kwa hiyo Tanzania ikizalisha chuma tani milioni moja tu kwa mwaka, inaweza kupata mapato ya fedha za kigeni kati ya dola milioni 600 mpaka dola bilioni moja kwa mwaka.
Jambo kubwa sana ambalo Tanzania imebahatika ni kwamba mashapo ya chuma yana madini mengine yenye thamani kubwa zaidi. Kwa mfano Vanadium ya Ludewa inauzwa tani moja dola 50,000 katika soko la dunia. Katika kila tani milioni moja ya chuma kutoka Ludewa, kuna tani 80,000 ya Vanadium. Tukiuza madini haya tunapata fedha za kigeni dola za kimarekani bilioni nne kwa mwaka.
#NingefanyaTofauti
Nchi yetu ina changamoto nyingi kiasi kwamba ni vigumu kuchagua ufanye ipi na uache ipi. Kiongozi mwenye maarifa huanza kutafuta fedha kwanza atekeleze majukumu mengine.
Viongozi wetu wa sasa wameamua kuanza kwa kutumia fedha za kodi au mikopo ghali yenye riba kubwa kutoka mabenki ya biashara ya nje. Wameanza na ujenzi wa reli wa dola bilioni saba, ununuzi wa ndege wa zaidi ya dola bilioni moja ( Dreamliner ‘Terrible Teen’) imenunuliwa kwa dola milioni 224 na hata ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Rufiji maarufu kwa jina la Stiglers Gorge litakalogharimu dola bilioni 3.5.
Ningekuwa na mamlaka ningeyafanya haya yote, lakini kabla ya kufanya hayo, ningeanza kwanza kwa kufanya jambo moja kubwa ambalo lingenipa fedha za kufanya hayo. Ningefanya tofauti.
Ningeanza na mradi wa Mchuchuma na Liganga kwa kuhakikisha kuwa uwekezaji unaanza mara moja na uzalishaji wa chuma na makaa ya mawe unafanyika bila kuchelewa. Ningehakikisha kuwa ndani ya miaka 2 tunaanza uzalishaji wa chuma, Vanadium na Titanium.
Mauzo ya Vanadium peke yake ni sawa na dola bilioni nne kwa mwaka ambapo kwa kuwa haya ni bidhaa ambatana na chuma maana yake 80% ya mapato haya yangekuwa ya nchi. Kwa hiyo mwaka wa kwanza tu wa uzalishaji ningeweza kupata dola bilioni 3.2. Kwa fedha hizo, tungejenga reli kuanzia Dar mpaka Dodoma kwa mara moja bila kuungaunga na kubakia na chenji ya dola bilioni moja ambazo ningeweza kujenga hospitali tano kubwa kama Mloganzila katika kanda tano za nchi; Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma na Arusha.
Ningeweza kujenga vyuo vya VETA kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini ( Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji ) kwani unahitaji shilingi bilioni 750 tu kujenga vyuo hivyo vilivyokamili na vifaa vya kutosha vijana kupata mafunzo.
Ningeweza kujenga vyuo vikuu vipya vitatu aina ya UDOM kwani UDOM moja ina thamani ya shs bilioni 800 tu. Haya ni mapato ya mwaka wa kwanza tu. Kumbuka kuwa tunaweza kuendelea kuchimba chuma tani milioni moja kwa mwaka kwa miaka 2000!
Kwanini hatuwekezi Mchuchuma na Liganga?
Kungoza nchi kunahitaji MAARIFA. Hakika #NingefanyaTofauti
Jitto zumbli kambwe... Uko bado hai...???
ReplyDeleteUtapata tabu tena sanaaaa......!!!!
Nasikia ulikwendaga kwa Lowasaa... Huyo si saizi yako.
Je ofisini bado unafunguwaga mlango na PS4 huwa unaichajigiiii!!!
Pole mwaya...!!! Kinga Lugola ameshasema wahamiaji wote mludigi makwenuuuuu... Unangojaga Nini wewe...Lauli yako mwanangu..Lugola ninjaaa huyoooo.....
Jitto zumbli kambwe... Uko bado hai...???
ReplyDeleteUtapata tabu tena sanaaaa......!!!!
Nasikia ulikwendaga kwa Lowasaa... Huyo si saizi yako.
Je ofisini bado unafunguwaga mlango na PS4 huwa unaichajigiiii!!!
Pole mwaya...!!! Kinga Lugola ameshasema wahamiaji wote mludigi makwenuuuuu... Unangojaga Nini wewe...Shauli yako mwanangu..Lugola ninjaaa huyoooo.....
Zitto na chama cha flashi mfukoni. .. Umeshapitwa na wakati... Wewe ulie tu
ReplyDelete