MBUNGE wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hali ya kisiasa ninayoendelea kwenye uchaguzi mdogo wa wabunge na madiwani inaasharia kitakachojiri kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kutaka wadau kuungana kuitetea demokrasia.
Zitto amesema hayo baada ya kutoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Ngoyai Lowassa leo asubuhi Julai 19,2018 alipokwenda kuzungumza naye na kusema udanganyifu unaotokea katika chaguzi hizo ndogo unatia wasiwasi hivyo kama wapinzani na wadau wengine wa demokrasia, huu ni wakati wa kuunda umoja imara kupinga uondoaji wa demokrasia na kuzuia kasi ya kukua kwa utawala wa amri.
Mchakato wa uchaguzi mdogo katika kata 77 na jimbo moja la Buyungu unaendelea na tayari CCM imeshapata madiwani 22 waliopita bila ya kupingwa baada ya kuwekewa upinzani na wagombea wa CCM au wasimamizi kuwaengua kwa madai ya kukosa sifa.
Wengine wameondolewa kwa kutoandika kwa usahihi neno “Zinjanthropus”, wako walioenguliwa kwa sababu walituhumiwa kwa mauaji, huku waengine wakienguliwa kwa madai ya kudai kazi zao ni wakulima wakati ni wa wafanyabiashara.
Aidha, wako walioenguliwa kwa madai kuwa si raia wa Tanzania na walioenguliwa kwa madai ya kutoa namba ya simu ambazo wasimamizi walidai si sahihi. Maamuzi hayo yameibua rufaa kutoka Chadema ambayo imesema wasimamizi wamekiuka sheria na taratibu za uchaguzi