MAREKANI wameiondoa Rwanda kwenye sheria ya Agoa, inayotoa msamaha wa kodi kwa bidhaa zenye kutoka nchi za Kusini ya Jangwa la Sahara.
Uamuzi wa Marekani umefuata baada ya Rwanda kuongeza kodi asilimia 1,000 ya mitumba inayotoka Marekani, kutoka dola 0.25 mpaka dola 2.50 mwaka 2016. Ifahamike kuwa mitumba inapotoka Marekani inasafirishwa kama misaada, hivyo Serikali ya Marekani haipati kodi. Serikali ya Rwanda inatoza kodi.
Biashara kwenda Marekani, Serikali ya Marekani haikuwa ikipata kodi stahiki kwa sababu ya msamaha, ila Rwanda inapata kwa kutoza kodi. Mitumba inakuza pato la taifa, wananchi wanamudu mavazi kwa bei rahisi.
Ukifanya uchambuzi kuhusu mgogoro wa kibiashara kati ya Marekani na Rwanda, unaona kwamba Rwanda wanapoteza, wakati sasa Marekani itapata kodi mpya endapo Rwanda watamudu kupeleka bidhaa nchini humo.
Kagame anaamua kuweka msimamo ili tu aivimbie Marekani. Na hili limekuwa tatizo sugu Afrika, viongozi kuamini kwamba kuyavimbia mataifa makubwa ulimwenguni ndiyo uzalendo. Kiongozi anawaumiza wananchi wake kwa sababu ya imani potofu, kwamba kuzigomea nchi za Magharibi ni kielelezo cha kupenda nchi na bara la Afrika.
Aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, aliwafukuza wakulima wa Kizungu waliokuwa wameshikilia uchumi wa nchi hiyo, kwa hoja ya kutaka mashamba yao yamilikiwe na maveterani wa vita ya ukombozi.
Hivi sasa Zimbabwe ni dhoofu kiuchumi. Mpaka leo ukimuuliza Mugabe kuhusu uamuzi huo, atajisifu uzalendo. Uchumi aliharibu, sarafu imegeuka karatasi.
Ni sababu Mugabe na viongozi wengine Afrika, humponda Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, kwamba aliwasaliti Waafrika kwa kukubali kuchangia madaraka na watu waliomtesa. Wao walitamani Mandela baada ya kushika madaraka alipe kisasi, awafukuze Wazungu na awabague. Kwao huo ndiyo uzalendo.
Kagame anaona kuzuia mitumba ndiyo uzalendo. Anasahau kwamba amevuruga fursa ya kibiashara yenye unafuu wa kodi, na anawapa wakati mgumu wafanyabiashara wa nchi yake. Afrika haiwezi kuendelea kwa falsafa za misuguano na ubabe. Huu ni ulimwengu wa fursa, vema kuzitumia kuliko kuziziba.
Ndimi Luqman MAL