Mkurugenzi wa habari, uenezi na uhusiano wa umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya amesema zaidi ya asilimia 70 ya migogoro ndani ya chama hicho imechangiwa na aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la uongozi chama hicho, Julius Mtatiro.
Kambaya amesema hayo ikiwa ni siku moja baada ya Mtatiro kujiengua CUF na kutangaza kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mtatiro ambaye alikuwa upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, alitangaza kuachana na chama hicho na kujiunga na CCM Agosti 11, 2018.
Kambaya amesema Mtatiro alipokuwa mwenyekiti wa mkutano mkuu alisababisha chama hicho kugawanyika kwa kutosikiliza maoni ya wajumbe wa mkutano huo na kuamua kuuendesha kibabe.
Ameongeza kuwa Mtatiro alipokuwa Naibu Katibu mkuu alikiingiza chama hicho katika mgogoro uliosababisha Hamad Rashid kufukuzwa uanachama baada ya kuhoji ubadhirifu wa fedha kiasi cha Sh300milioni katika uchaguzi mdogo wa ubunge Igunga.
“Hakuna kitu ambacho Mtatiro amekifanya kwenye chama hiki, kubwa zaidi amesababisha migogoro. Wanasiasa wapambanaji hawakimbii migogoro ndani ya vyama vyao bali wanakaa humo humo mpaka migogoro itakapokwisha” amedai Kambaya.
Kambaya ambaye yupo upande unaomuunga mkono mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kuwa; “Tazama Sophia Simba hakukimbia CCM sambamba na Nape Nnauye (mbunge wa Mtama-CCM). Hata Mnyika (John-Mbunge wa Kibamba-Chadema) hakukimbia chama hicho.”