ATCL Yafunguka Sababu za Dreamliner Kutoonekana Hewani

ATCL Yafunguka Sababu za Dreamliner Kutoonekana Hewani
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limezungumzia kutosafiri kwa ndege yake mpya aina ya Boeing 787-7 Dreamliner, iliyoanza kazi mwishoni mwa mwezi uliopita.

Tangu ilipoanza safari zake Julai 29, ndege hiyo imekuwa ikifanya safari kati ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza kila siku asubuhi na jioni.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Ladislaus Matindi alisema juzi kuwa, hakuna ndege yao ambayo imekwama mahali popote na hata Dreamliner ambayo shirika limeisimamisha kwa makusudi kutokana na matakwa ya kiufundi.

“Tunazo ndege nne, tatu aina ya Bombardier Q400 zinaruka na kufanya safari zake kama kawaida, Dreamliner tumeisimamisha sisi wenyewe kwa ajili ya matakwa ya kiufundi, kwa hiyo iko chini kuanzia jana (Agosti 14), leo (Agosti 15) na kesho (Agosti 16),” alisema Matindi wakati akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam, juzi.

Alisema nia ni kuangalia sehemu za marekebisho katika ndege hiyo ikiwemo suala la WiFi ambayo inatakiwa kufanyiwa marekebisho madogo na mambo mengine yanayohusiana na uendeshaji kwa kuwa safari zinazofanyika sasa ni za majaribio na mafunzo kwa marubani.

“Ndege ilisimamishwa ili kufanyia marekebisho ambayo yanatakiwa katika uendeshaji. Hayo yanayosemekana siyo kweli na kesho (jana) tutakuwa tumemaliza na tutaendelea na safari za Dreamliner,” alisema.

Awali, baadhi ya taarifa zilisambaa mitandaoni zikidai ndege hiyo ilikuwa na matatizo yaliyosababisha abiria waliotakiwa kusafiri nayo kukwama hadi wakatafutiwa ndege nyingine.

Matindi alisema ATCL walipanga kuwa matengenezo yangefanyika baada ya wiki tatu, lakini mafundi waliomba yafanyike mapema kwa sababu wanakaribia kuondoka, hivyo ikabidi shirika lifanye uamuzi wa ghafla.

“Marekebisho yalifanywa baada ya kukamilika kwa safari moja ya kutoka Mwanza kurudi Dar es Salaam, hivyo hakuna abiria yeyote aliyetelekezwa wala kushushwa uwanja wa ndege kama inavyoelezwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mawasiliano wa ATCL, Joseph Kagirwa alisema abiria wote ambao walitakiwa kusafiri na Dreamliner kwa safari zao, baadhi yao walisafirishwa na Bombardier na wengine walipandishwa katika ndege za mashirika mengine.

“Tulifanya mawasiliano na abiria wetu siku moja kabla, kila mmoja alipigiwa simu kuelezwa dharura iliyojitokeza, hakuna mtu aliyetozwa nauli zaidi na ofa zetu zinaendelea kama kawaida,” alisema Kagirwa.

“Kesho Dreamliner inarejea katika safari zake kama kawaida na ndege itakuwa imejaa.”

Abiria waliokwama

Baadhi ya wasafiri ambao walitarajia kusafiri na ndege hiyo kutoka Kilimanjaro kwenda Dar es Salaam juzi, walilazimika kukaa uwanjani kwa zaidi ya saa nane.

Abiria waliozungumza na gazeti hili walilalamikia kutopewa taarifa mapema juu ya ndege hiyo iliyotakiwa kuondoka uwanjani hapo saa sita mchana, lakini haikufika.

“Tuko uwanjani hapa toka saa nne na tulitakiwa tuondoke kuelekea Dar es Salaam majira ya saa sita mchana, lakini hadi sasa bado hatujaondoka,” alisema mmoja wa abiria ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Baadaye abiria huyo alisema waliondoka kwa makundi kwa kutumia ndege za mashirika mengine.

Abiria huyo alisema kundi la kwanza liliondoka uwanjani hapo saa 12 jioni na la mwisho liliondoka saa mbili usiku.

“Baadhi ya abiria wameshasafiri kwa kutumia ndege za kampuni nyingine, lakini abiria 15 kati ya 50 tuliotarajia kusafiri kwa ndege hiyo bado tupo uwanjani, hatujui hatima yetu,” alisema abiria huyo kabla ya baadaye kusema walifanikiwa kuondoka saa mbili usiku.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad