KAMA ulikuwa unadhani wakali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ally Salehe Kiba ‘AliKiba’ ndio wenye mijengo ya maana Bongo utakuwa umechelewa kidogo kujua, yupo Mbongofleva mwingine Ambwene Yessaya ‘AY’ ambaye amewaziba midomo mastaa hao kwa kununua mjengo wa maana maeneo ya Calabasas, California nchini Marekani, Ijumaa linakupa ‘full’ stori.
Mjengo huo eneo la mbele.
TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na staa huyo aliyewahi kutamba na nyimbo nyingi ikiwemo Zigo, tangu afunge ndoa na mwandani wake, Rehema Sudi ‘Remmy’, Februari mwaka huu, makazi yake yamekuwa ni nchini humo.
“Mwanzoni zilianza kusambaa picha za mjengo wa ghorofa moja zikimuonesha eneo la mbele AY akiwa sambamba na mwanamke mmoja aliyefahamika kama Sheila Kiwanuka ambaye kwenye akaunti yake alijitambulisha kama muuzaji wa majengo mbalimbali,” kilisema chanzo.
NI CALABASAS
Chanzo kinazidi kutiririka kuwa, katika moja ya picha hizo, zinawaonesha wawili hao wakiwa katika moja ya bwawa la kuogelea katika mjengo huo ambao upo mjini Calabasas ndani ya Los Angeles.
“Ukiangalia katika mjengo huu, ni mazingira yake yamefunikwa na miti mizuri ikiwemo ya kupandikizwa, yaani kifupi Calabasas ni kama eneo lililozungukwa sana na milima iliyoambatana na miti kwa hiyo hapo jamaa ameula.”
JINSI ALIVYOUPATA MJENGO HUO
Chanzo kiliiambia Ijumaa kuwa, jambo la kumiliki mjengo nchini humo si la kitoto hivyo kwa hatua aliyofanikiwa AY ni kubwa na ni mfano wa kuigwa na kila mtu mwenye kupenda maendeleo hasa kwa hawa vijana.
Nyumba ya Alikiba.
“AY ameweza kuwapa nguvu vijana wengi kupitia muziki, ukiangalia hivi sasa Muziki wa Bongo Fleva upo levo nyingine za kimataifa lakini hiyo yote ni juhudi zake za kuwa alikuwa wa kwanza kupata chaneli, kwa hiyo nategemea hata hili la kumiliki nyumba Marekani litawapa nguvu wengi.”
GHARAMA ZAKE
“Kwa kawaida nyumba nyingi za maeneo ya Calabasas gharama zake huanzia dola 300,000 (zaidi ya milioni 685 za Kitanzania) na kwa mjengo tu wa AY thamani yake inaanzia dola 500,000 (zaidi ya bilioni 1.1 za Kitanzania) na kuendelea,” kilisema chanzo.
YUPO KARIBU NA BILL BLANKS, DR. DRE
Chanzo kilizidi kumwaga data kuwa, mbali na AY kuchagua kununua mjengo eneo hilo, kikubwa kilichomvutia ni uwepo wa mastaa wengi wakubwa wanaomzunguka.
“Anaishi na mastaa wakubwa duniani akiwemo mkongwe wa filamu duniani, Billy Wayne Blanks ‘Billy Blanks’ aliyewahi kutamba na filamu nyingi za mapigano kama vile TC 2000, The King of The Kickboxers pamoja na Back in Action.
“Pia anaishi na mkongwe mwingine wa Muziki wa Hip Hop, Andre Romelle Young ‘Dr. Dre’ ambaye pia ni Mkurugenzi wa Headphones za Beats by Dre zinazotikisa duniani kwa hiyo utaona namna gani AY amezungukwa na mastaa.
NI RAHISI KUMTEMBELEA JAY Z, BEYONCE
“Jay Z (Shawn Carter) anaishi na mkewe, Beyonce Knowles katikati ya Jiji la Los Angeles ambapo kutoka anapoishi AY na Remy yaani Calabasas mpaka jijini hapo ni mwendo wa kilomita 47 sawa na dakika 49 tu,” chanzo kiliweka nukta.
HUYU HAPA AY
Ili kuju mengi zaidi kuhusu mjengo huo, Ijumaa lilimsaka na kufanikiwa kumfikia AY kwa njia ya WhatsApp moja kwa moja kutoka Calabasas ambapo alikiri kumiliki mjengo huo.
“Ni kweli nimefanikiwa kupata nyumba hapa Calabasas na ndipo yatakuwa makazi yangu,” alisema AY na alipoulizwa kuhusiana na gharama hakutaka kuweka wazi.
Nyumba ya Diamond.
AMEWAFUNIKAJE KIBA, DIAMOND?
Kwa wasanii wa Bongo Fleva, AY anakuwa msanii wa kwanza kumiliki nyumba Marekani, taifa lenye nguvu kubwa duniani.
Mbali kuwa wa kwanza, anakuwa msanii wa kwanza kumiliki nyumba yenye thamani kubwa nje ya nchi tofauti na kina Diamond na Kiba wenye mijengo yao inayotajwa kuwa na thamani ndogo.
MJENGO WA KIBA, DIAMOND
Kiba anamiliki mjengo maeneo ya Tabata Sanene jijini Dar ambao thamani yake inadaiwa kuwa milioni 250 wakati Diamond mjengo wake ulipo maeneo ya Tegeta-Madale, jijini Dar unadaiwa kumgharibu kiasi cha shilingi milioni 400.