Baada ya Kutangaza Ndoa ya Wema Sepetu Steve Nyerere Atangaza Ndoa ya Wellu Sengo

Steve Nyerere Atangaza Ndoa ya Wellu Sengo
UKISIKIA mtoto anasema hadithi… hadithiii na wengine kuitikia ‘hadithi njoo utamu kolea’, basi ujue simulizi inafuata. Sharti lake ni kukaa kimya na kusikiliza kwa makini. Alichokisema hivi karibuni Msanii wa vichekesho Bongo, Steve Nyerere, ndani ya Ukumbi wa Alfa uliopo Morocco jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe ya harusi ya msanii mwenzake Jimmy Mafufu ni kama kuwaandaa watu wasubiri utamu ukolee.

TUKUMBUSHANE KWANZA

Ikumbukwe kwamba Steve Nyerere yuko katika maisha ya ndoa na kwamba amekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanamama mwingine kutoka Bongo Muvi, Wellu Sengo na kufanikiwa kuzaa naye mtoto mmoja.

Mara nyingi uhusiano huo na Wellu umekuwa ukizua figisufigisu nyingi ndani ya ndoa ya mchekeshaji huyo kiasi cha kuitikisa; chupuchupu kuivunja. Aidha, Steve Nyerere mwenyewe amekuwa akiuzima ‘moto’ wa wivu wa mkewe kwa kueleza kuwa kilichotokea kwa Wellu kilikuwa sawa na ajali kazini.

STEVE NYERERE AIBUKA NA HILI

Wakati watu waliokuwa ukumbini wakiendelea na sherehe ya harusi ya Jimmy aliyemuoa mrembo aitwaye Upendo Meja; mara zamu ya Steve Nyerere kusema chochote ikawadia ambapo alifunguka haya: “Samahani kwanza, naomba kuuliza, “hivi Wellu yumo humu?” Watu wakaanza kupepesa macho ukumbini kumshuhudia msanii huyo ambaye aliinuka na kumfuata mzazi mwenzake mbele ya waalikwa.

Steve akamwanga jingine tena laivu: “Mama ndoa yetu na sisi inakaribia anza kujiandaa,” ukumbini kukasikika shangwe kuonesha kwamba watu wamefurahia na kwamba wanasubiri utamu ukolee. Hata hivyo, mke wa Steve Nyerere ajulikanaye kwa jina moja la Zawadi mara kadhaa amekuwa akimtuhumu bila kumtaja jina Wellu kwamba anamvunjia ndoa yake.

“Steve ataenda popote lakini atarudi tu, kuna wadada wenye maisha magumu wanataka kuwa na maisha bora ndiyo maana wanamsumbua sana mume wangu,” inasomeka nukuu ya hivi karibuni ya mke wa Steve Nyerere inayopatikana mitandaoni. Kwa upande wake Steve Nyerere alipozungumza mwezi Juni mwaka huu, aliliambia gazeti dada la hili, Amani kuwa:

”Ni kweli nimezaa na Wellu lakini watu lazima wajue kwamba kuzaa na mtu siyo kuoa, hivyo sidhani kama nitamuoa Wellu,” Haya! Ile sauti ya hadithi, hadithiii, ndiyo hiyo kaitoa Steve Nyerere; kazi yetu ni kumuitikia “Hadithi njoo utamu kolea.” Tuisubiri hiyo ndoa.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad