ACHANA na habari za La Liga. Straika namba moja wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta anaweza kuwashangaza mashabiki wake kwa kutua Ligi Kuu ya England muda wowote kuanzia sasa.
Baba mzazi wa mchezaji huyo tajiri zaidi nchini, Mzee Ally Samatta amefichua siri kubwa aliyoelezwa na mwanae huyo kuwa yupo katika mipango mizito ya kujiunga na timu mbili za England ambazo ni Leicester City na West Ham United, huku akisisitiza lolote linaweza kutokea.
Samatta mwenye miaka 25, anayekipiga katika kikosi cha KRC Genk cha Ubelgiji, alitua hapo Januari, 2016 akitokea TP Mazembe ya DR CongoAkizungumza na Championi Jumatano, Mzee Samatta alisema kuwa licha ya mtoto wake kudaiwa kutakiwa na Levante, lakini kwa upande wake alimdokeza ana mpango wa kwenda Leicester City kutokana na kushawishiwa na rafiki yake waliocheza wote Genk kabla ya kutimkia timu hiyo, Wilfred Ndindi.
“Kiukweli hizo taarifa nimezisikia kama watu wengine wanavyosema kwamba sijui hao Levante ya Hispania, wengine wanaitaja Borussia Dortmund ya Ujerumani kuwa nao pia wamekuwa wanamuhitaji, lakini mimi nimeongea naye mwenyewe na alichosema ni kwamba kama mimba ndiyo imetunga basi tusubiri tuone kitakachotokea,” alisema Mzee Samatta na kuongeza.
“Uzuri Samatta kuna watu ndiyo wanamsimamia na hata hilo suala la Levante ndiyo maana akasema tusubiri kitakachotokea kwa sababu mwenyewe yupo kwenye mipango ya kwenda England na timu nilizoambiwa ni Leicester na West Ham lakini Leicester ndiyo sana kwa sababu pale kuna rafiki yake kutoka Nigeria, Wilfred Ndidi ambao walicheza pamoja Genk ila amenisisitiza kwamba atakayekuwa na kisu kikali ndiye atakula nyama.”
Mpaka sasa akiwa na Genk, Samatta amecheza jumla ya mechi 54, za Ligi Kuu Ubelgiji pamoja na michezo 12 ya mashindano ya Europa Ligi. Msimu uliopita haukuwa mzuri kwa Samatta kutokana na kusumbuliwa na goti jambo lililomfanya acheze mechi 35, lakini msimu huu yupo fiti na tayari ameanza kazi.