Staa wa muziki wa Injili, Bahati Bukuku (pichani), ameingia kwenye skendo nzito kufuatia kusakwa nchini Kongo kwa tuhuma za utapeli, Amani linakupa habari kamili.
TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo makini kutoka Kongo kilieleza kwamba, Bahati alitakiwa kwenda kufanya tamasha kwenye mkutano wa Injili ulioandaliwa na Askofu Wamwabi Francine wa Kanisa la Mlima wa Ushindi Mei, mwaka huu lakini hakutokea.
“Unajua alitakiwa kwenda kufanya huduma Kongo tangu mwezi wa tano lakini hakwenda na alikuwa ameshachukua fedha za watu, sasa kitendo hicho kimewakasirisha sana wahusika hivyo anasakwa kwa udi na uvumba nchini Kongo,” kilieleza chanzo.
TUJIUNGE KONGO
Ili kuujua ukweli wa habari hizo, Amani lilifanya jitihada za kumtafuta Mwenyekiti wa Baraza la Wanamuziki lililopo Bukavu nchini Kongo, Wato Mukambilwa Adam ambaye alisema wamepokea malalamiko hayo na kuwasiliana na viongozi wa wanamuziki wa Injili Bongo.
Aliendelea kueleza kwamba, Askofu Wamwabi kupitia kwa Askofu Ben Cale
aliyemuunganisha na Bahati Bukuku alikuwa ameandaa mkutano ambao ulifanyika Mei, mwaka huu na walielewana kwamba malipo yake ni dola 2000 (zaidi ya shilingi milioni 4.5).
ATUMIWA ADVANSI
Alisema, baada ya kuelewana alitumiwa advansi kwa njia ya Western Union ambayo ni dola 1000 zilizobaki kutokana na mkataba walikubaliana kumalizana baadaye.
“Siku ya mkutano ikiwa imekaribia, Bahati akawa anapigiwa simu ili kuambiwa kwamba anatumiwa tiketi ya ndege lakini simu yake hiyo ya mkononi ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa licha ya kutafutwa mara kadha wa kadha.
“Mkutano ulifanyika na watu walikasirishwa sana kuona walivyotangaziwa kwamba Bahati atakuwepo walidanganywa, kitendo hicho kilimuudhi Askofu Wamwabi na kueleza ukweli kwamba mwimbaji huyo alimtapeli.
“Askofu Wamwabi alieleza kwamba alifanya uchunguzi wake na kujua kuwa Bahati amemtapeli na siyo kwamba alikosa ndege kama alivyokuja kujitetea baadaye,” alisema Wato.
APIGWA MARUFUKU KONGO
Wato alieleza kwamba kutokana na kitendo hicho alichofanya Bahati na aliyemuunganisha ni kiongozi wa Serikali pia na huyo askofu ana nguvu sana nchini Kongo, muimbaji huyo amepigwa marufuku kukanyaga ardhi ya nchi hiyo.
“Askofu Caleb ambaye alimuunganisha alifikia uamuzi huo kiserikali na imewekwa muhuri na viongozi wote kwa kila ngazi kwa hiyo hata akirudisha hela haitoshi, maamuzi yaliyotolewa ni kwamba ni marufuku Bahati kukanyaga Kongo.
“Wakati Askofu Wamwabi anatoa taarifa hiyo alieleza kwamba maamuzi hayo yalifikiwa ili yawe fundisho kwa wengine kwani kuna wanamuziki wengi wa Injili kutoka Tanzania wamekuwa wakipokea fedha za kwenda kutoa huduma ya uimbaji lakini hawafiki, hivyo Bahati atakuwa fundisho kwa wote.
“Hivi karibuni Bahati alipigiwa simu na kueleza kwamba atarudisha hizo dola 1000 lakini mpaka sasa hajarudisha yuko kimya hivyo malalamiko yote tumeyapeleka kwa Chama cha Muziki wa Injili cha Tanzania Music Foundation ili kiweze kushughulikia na kutambua kwamba muimbaji huyo hatakiwi Kongo,” alimaliza Wato.
CHAMA CHA INJILI BONGO CHANENA
Akizungumza na Amani, Rais wa Tanzania Music Foundation, Dk. Donald Kissanga alikiri kupokea malalamiko hayo kutoka kwa Baraza la Muziki la Kongo na wanaendelea kuwasiliana nao ili kubaini ukweli wa hilo suala la Bahati kutapeli.
“Tumepokea malalamiko kuhusu Bahati kupokea fedha na kutokwenda kufanya huduma Kongo, tunafuatilia ili tusuluhishe yaishe maana tumekuwa tukisuluhisha matatizo mengi sana na yanaisha kwa sababu hii ya kufungiana siyo vizuri kwa waimbaji wetu,” alisema Dk. Donald.
BAHATI ANASEMAJE?
Katika kuujua ukweli wa tuhuma hizo, Amani lilimtafuta Bahati ambaye alikuwa na haya ya kusema;
“Hao watu tulikubaliana kwenye mkataba kwamba ninaenda kuhudumu katika mkutano na siyo tamasha lakini wao wakawa wanatangaza kwamba naenda kwenye tamasha kitu ambacho ni kinyume na makubaliano yetu.
“Pia katika mkataba tulikubaliana wao watanitumia tiketi ya ndege lakini hawakutuma, sasa mimi ningeenda kwa muujiza gani? Watanzania wanajua tabia yangu sijawahi kumtapeli mtu maana mimi ni mtumishi wa Mungu.