Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha CUF Julius Mtatiro amejivua uanachama wa chama hicho nakujiunga na Chama cha Mapinduzi CCM huku akisema kuwa huu ni wakati wake wakwenda kutumia vipaji vyake kikamilifu pia kuwa balozi mkubwa wa Rais Magufuli Ndani na nje ya Nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam amesema kuwa ameamua kuchukua uamuzi huo kwa kuwa jukwaa alilokuwa analisimamia katika siasa kwa miaka kumi limeshindwa kumpa nafasi yakuifanyia nchi yake maendeleo.
"Nimeamua kwa dhati kuanzia hivi sasa, kuwa mmoja wa mabalozi wakubwa wa Taifa langu na balozi mkubwa wa Rais wa Taifa hili, na kazi hiyo ntaifanya ndani na nje ya nchi na ntafanya hivyo kwa vitendo na maneno na wala sitasita.
"Nimejiridhisha kwa hitaji la Nafsi yangu kwamba nijiunge na Chama cha Mapinduzi CCM, nawajulisha watanzania rasmi kuwa nimeanza mipango ya kutekeleza hili mara moja.
"Siendi CCM kutafuta nafasi na ukuu,uamuzi niliofanya ni uamuzi wa kutafuta jukwaa sahihi lakufanya siasa katika kipindi cha mbele cha maisha yangu." Amesema Julius Mtatiro na kuongeza;
"Maswala ya misimamo yangu ya sera na ilani za CUF na misimamo ya CUF hayo yanabakia CUF."