Chadema wajitoa uchaguzi Songoro jijini Arusha
0
August 12, 2018
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo mchana Jumapili Agosti 12, 2018 wametangaza kujitoa katika uchaguzi kata ya Songoro wilayani Arumeru kwa madai kuwa mawakala na mgombea wao wamepigwa na vijana wanaodaiwa kuwa makada wa CCM.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema baada ya mashauriano kati ya chama na mgombea, Godluck Nanyaro wameona hakuna sababu ya kuendelea na uchaguzi.
“Tumeamua kuwaondoa vituoni mawakala wetu katika vituo 14 kutokana na kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu,” amesema.
“Mgombea amepigwa, mawakala wanapigwa vituoni na wengine walizuiwa kuingia vituoni muda mrefu huku upigaji kura ukiendelea.”
Nassari akiwa pamoja na Katibu wa Chadema mkoa Arusha, Isaya Mungure amesema mapema leo asubuhi katika eneo la Shule ya Msingi Urisho, mawakala wao walizuiwa.
Amebainisha kuwa Nanyaro alikwenda kushuhudia hali hiyo katika kituo cha Urisho A lakini alivamiwa na vijana aliodai ni wa CCM na kumshushia kipigo jambo lililowalazimu polisi kuingilia kati na kuwapeleka wote kituoni.
Msimamizi uchaguzi Arumeru Mashariki, Christopher Kazeri amesema Chadema waliondoa mawakala wao saa 5 asubuhi bila kueleza sababu za kujitoa.
Amesema vyama vina hiari ya kujitoa lakini hatua hiyo haipotezi uhalali wa uchaguzi kuendelea.