Chadema Yaitumia Barua NEC

Chadema Yaitumia Barua  NEC
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kikilalamikia kile kilichotokea Korogwe Vijijini, ambapo mgombea wa ubunge kupitia (CCM), Timotheo Mzava amepita bila kupingwa.


Barua hiyo imeandikwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt. Vincent Mashinji imekwenda kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dkt. Athuman Kihamia na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Korogwe Vijijini, Dkt. George Nyaronga.

Dkt. Mashinji ametuma barua hiyo baada ya Dk Nyaronga kumtangaza mgombea wa CCM, Timotheo Mzava kupita bila kupingwa.

Barua imesema kuwa, “Rejea mazungumzo yetu ya simu awali leo (jana) saa 6:03 mchana na ukanirudia saa 06:06 kuhusu msimamizi wa uchaguzi Korogwe kutopokea fomu ya mgombea ubunge kupitia Chadema, Amina Ally Saguti ambaye alikuwapo muda wote leo (jana) kuanzia saa 4:00 asubuhi ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Korogwe Vijijini, jambo ambalo uliahidi kulighulikia,”

Dkt. Mashinji ameongeza kuwa, “Nilikurejea tena saa 09:47 jioni kukujulisha kuwa bado msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Korogwe Vijijini hajapokea fomu za mgombea kupitia Chadema na ukanirejea tena saa 09:55 ukinieleza kuwa unashughulikia”.

Katika barua hiyo, Dkt Mashinji ameendelea kusema, “Katika mazingira hayo, tunaitaka ofisi yako na Tume iingilie kati suala hili kubwa la uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili mchakato urejewe kuruhusu mgombea wetu wa Chadema na wengine waliochukua fomu za uteuzi waweze kurejesha fomu hizo kwa ajili ya uteuzi”.

Akizungumza  msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Korogwe, Dkt. George Nyaronga amesema mgombea wa CCM ambaye ni Mzava amepita bila kupingwa baada ya muda wa mwisho wa kurejesha fomu leo Agosti 20, 2018 kuwa peke yake.

Jimbo la Korogwe Vijijini limekuwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Stephen Ngonyani maarufu kama Maji Marefu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad