Rais John Magufuli ametumia hafla ya kuapishwa kwa wakuu wa mikoa, manaibu katibu wakuu na makatibu tawala wa mikoa kukumbusha majukumu yao katika maeneo ya utendaji ambapo amedai mkoa wa Dar es salaam umeshindwa kufikia malengo kwenye ukusanyaji wa mapato.
Rais ameusifu mkoa wa Dodoma kwa kuongoza kwa ukusanyaji mapato, ikiwa ni siku chache baada ya kupandishwa hadhi na kuwa jiji.
“Dodoma inaogoza kwa makusanyo mengi, Sh24.5 bilioni. Sasa unaweza kujiuliza, Dodoma kuna nini?” alisema Rais.
“Yule mkuu wa mkoa wa Dodoma, RAS (katibu tawala), mstahiki meya na wananchi wa Dodoma wana genes za namna gani ukilinganisha na Dar es Salaam ambayo ina population (idadi) ya watu 5.5 milioni?”
Alisema mkoa wa Dar es Salaam uliwekewa malengo ya kukusanya Sh12 bilioni lakini hauklufikisha.
“Sasa unaweza ukajua kwamba hapa Dar es Salaam kuna upigaji tena wa nguvu. Lakini viongozi wapo.”
Pia alisema hata wilaya ya Kinondoni ambaye aliyekuwa akiiongoza, Ali Hapi amempandisha cheo na kuwa mkuu wa mkoa, ilikuwa ya mwisho.
“Sasa nikawa najiuliza sijui nimtumbue hapa hapa au,” alisema Rais Magufuli huku akikuna kichwa.
“Kweli wala sifichi, nikasema wilaya ilikuwa ya upinzani ile. Lakini hivi vitu vinatia aibu.”
Huku akizungumzia majiji mengine, alikosoa pia jiji la Mbeya akisema limeshika nafasi ya mwisho kati ya majiji sita nchini.
“Yaani jiji nililotangaza miezi miwili mitatu iliyopita ndio linaongoza! Nimejiuliza sana, labda tuweke mikakati ya kufanya; jiji linaloshindwa kukusanya linashushwa chini. Utaitwaje jiji wakati hata hujui kukusanya?” alihoji.
Alizitaja pia halmashauri za Mbulu na Mbinga akisema zimekuwa za mwisho katika ukusanyaji wa mapato, huku akiwataka wakuu wa mikoa kusimamia kazi hiyo.
“Wakuu wa mikoa ni kila kitu, hakuna mahali popote panaweza kukukwamisha. You are everything,” alisema.
“Sasa mimi huku Rais ninakazania mapato huku, wewe rais wa mkoa ule unashindwa kusimamia mapato, kwa nini nisijiulize kwamba hufai?
“Survival ya nchi hii ni mapato, fedha zinazokusanywa ziende kwenye miradi ya maendeleo ili nchi iende mbele. Hapa Dar es Salaam, wala siyo siri, wakikutana kwenye vikao, madiwani kama wamekaa siku moja wanalipana siku nne. Kila mmoja anajua. Wakikutana siku mbili zitakazojazwa pale ni siku nne. PCCB wapo. Unategemea utapata hela gani kwa maendeleo?”
Alisema kutokana na hali hiyo kero za wananchi wakiwemo wafanyabiashara ndogo hukosa nafasi za kufanya biashara licha ya kuwepo kwa viongozi.
Dar Kuna Upigaji Tena wa Nguvu Lakini Viongozi Wapo tu! – Rais Magufuli
0
August 02, 2018
Tags