DCI Afunguka Sakata la Kumkamata Aliyekuwa Mkurugenzi NIDA

DCI Azungumzia Sakata la Kumkamata Aliyekuwa Mkurugenzi NIDA
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz amesema wanayafanyia kazi maagizo ya kumkamata mkurugenzi mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu.

Maagizo hayo yalitolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola siku mbili zilizopita akitaka Maimu kukamatwa kwa kosa la tuhuma za kula njama na kuisababishia hasara Serikali ya Sh4.6 bilioni.

Mbali na Maimu, wengine waliotakiwa kukamatwa juzi kabla ya saa 12:00 jioni kwa kosa hilo ni mmiliki wa kampuni ya Gotham International Ltd, Gwiholoto Impex Ltd na Ms Aste Insurance Broker Company Ltd.

Wamiliki wa kampuni hizo tatu walikamatwa na polisi waliokuwa katika ofisi za wizara hiyo juzi. Maimu hakuwapo katika mkutano na waziri, bali alikuwapo katika mahojiano naye Agosti 3.

DCI Boaz jana alisema serikali inajitahidi kuhakikisha kuwa taasisi za umma zinaheshimu haki za binadamu na uzalendo kwa kutumia vyema mali zilizopo.

Alisema wale ambao wamekuwa wakifanya ubadhirifu wa mali za umma lazima wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

 Alisema Waziri ana dhamana ya Wizara na pia ni cheo cha kisiasa hivyo lazima aweke msimamo katika masuala hayo na akimwagiza yeye analenga kuwataka vyombo vya dola vitoe vijana wake kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Alisema wakikamilisha utaratibu kuwakamata watuhumiwa, watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yao na endapo watapata dhamana wataendelea kufanya upelelezi na kwamba wakiendelea kushikiliwa, upelelezi utaendelea hadi kuwabaini waliohusika na ubadhirifu huo.

Alisema kuendelea kufanya uchunguzi wakati watuhumiwa wakiwa mahakamani kunalenga kupata uthibitisho wa kina na kukusanya vielelezo ili kujua ni nani aliyehusika.

‘’Suala la uhujumu uchumi wa fedha za serikali linakuwa na mtandao mkubwa ambao mara nyingi kuwapata waliohusika kwa asilimia 100 ni ngumu kwa sababu wanashirikiana na watu ambao kuwafahamu inahitaji uchunguzi wa kina na wa muda mrefu, kuwapata walioshirikiana na wakurugenzi hao kufanya ubadhirifu,’’ alisema.

Agosti 15, 2016 mtuhumiwa Maimu, Kayombo na wafanyakazi wengine NIDA, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 1.16.

Wafanyakazi hao wa Nida ni Meneja Biashara, Avelin Momburi, Benjamin Mwakatumbula (Kaimu Mhasibu Mkuu), George Ntalima (Ofisa Usafirishaji), Sabina Raymond (Mkurugenzi wa Sheria) na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Joseph Makani.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 15 hadi 19, mwaka 2010 makao makuu ya NIDA wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi zao waliidhinisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya Dola za Marekani 2,700,00 bila ya kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania, kinyume na kifungu 19.3 cha mkataba kati ya NIDA na GIL, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 3,969,000.

Pia walidaiwa kati ya Juni 3 na 5, 2013 katika makao makuu hayo walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani milioni 1.8, bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 106,346,000.

Pia Juni 20, 2014 katika makao makuu hayo, waliidhinisha tena malipo ya Dola za Marekani 675,000 kwa GIL bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 42,471,000.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo mengine ya Sh milioni sita kwa GIL bila ya kupiga hesabu kwa kutumia viwango vya kubadilishia fedha hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 14, 661,676.76.

Inadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 15, 2010 na Mei 16, 2015 katika makao makuu hayo ya NIDA kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni waliisababishia NIDA kupata hasara ya Sh 167,445,676.76.

Anadaiwa Aprili 16, 2012 katika makao makuu ya NIDA, Ndege akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Broker ambayo imeingia mkataba na NIDA wa kutoa huduma za bima, kwa nia ya udanganyifu aliwasilisha hati ya malipo yenye taarifa za uongo NIDA akionyesha kampuni yake inastahili kulipwa Sh 22,582,281 kwa huduma za bima iliyoitoa huku akijua taarifa hizo za uongo na zilikuwa na lengo la kumdanganya mwajiri wake.

Mkurugenzi huyo wa NIDA, Mwakatumbula na Ndege, wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Januari 4,2013 makao makuu ya NIDA waliisababishia hasara ya Sh 55,312,800.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa pia kati ya Januari 29 na 30, 2013 katika makao makuu hayo walitumia madaraka yao vibaya kuidhinisha malipo ya Dola za Marekani milioni mbili kwa IRS Corporation Berhad.

Ilidaiwa mapendekezo ya utaratibu mpya wa haraka wa upatikanaji wa vitambulisho na vifaa bila ya kufanya marekebisho ya mkataba ulioko kati ya NIDA na kampuni uliiwezesha IRIS kupata faida ya fedha hizo.

Mwakatumbula, Ntalima na Kayombo wanadaiwa kati ya Juni 4 na 6, 2013 makao makuu waliisababishia NIDA hasara ya Sh 45,515,961.

Maimu na Sabina wanadaiwa kati ya Agosti 3, 2010 na Novemba 7, 2011 katika makao makuu ya NIDA wakati wakitekeleza majukumu yao, walitumia madaraka yao vibaya na kuiwezesha GIL kupata faida ya Sh 901,078, 494 na kuisababishia NIDA hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad