Dereva wa Kigwangalla aachiwa kwa dhamana


Jeshi la Polisi mkoani Manyara limemuachia kwa dhamana Juma Salehe (59), dereva wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla na kumtaka kuripoti polisi kila siku hadi uchunguzi wa ajali utakapokamilika.


Salehe alikuwa akiendesha gari la waziri huyo lililopata ajali Agosti 4, 2018 eneo la Magugu mkoani Manyara na kusababisha kifo cha aliyekuwa ofisa habari wa wizara hiyo, Hamza Temba.


Baadhi ya waliokuwemo katika gari hiyo walipata majeraha sehemu mbalimbali mwilini, akiwemo Dk Kigwangalla aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).


 Kamanda wa polisi mkoani humo, Augustine Senga amesema, “tulikuwa tumemshikilia kama kawaida kwa kusababisha ajali na sasa yupo nje kwa dhamana anakuja kuripoti hapa ofisini.”


Amesema uchunguzi ukikamilika faili litapelekwa kwa mwanasheria wa Serikali kwa taratibu nyingine za kisheria.


Kamanda Senga amesema gari hilo lilikuwa na watu sita, mmoja alifariki dunia na watatu kujeruhiwa huku wawili wakitoka salama.


Amesema chanzo cha ajali hiyo ni twiga kukatiza barabarani ghafla na dereva katika jitihada za kumkwepa aliyumba kushoto na kulia na kusababisha gari hilo kupinduka.


Amewataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni mwandishi wa habari Michael Mlingwa (30) na msaidizi wa waziri huyo, Ramadhan Magumba (30).


Amesema katibu wa Dk Kigwangalla, Ephraim Mwangombe (47) na Salehe hawakupata jeraha lolote kwenye ajali hiyo.


Amesema mpaka sasa Magumba amelazwa hospitali akiendelea na matibabu baada ya kuumia shingo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad