Na Is-haka, Zanzibar.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Dk.Bashiru Ally amesema CCM inaendelea kuimarika na hakuna Chama chochote cha kisiasa nchini kinachoweza kushindana nacho katika uringo wa siasa za ushindani wa sera za maendeleo kwa wananchi wa makundi yote.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kuwasili kisiwani Pemba katika mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha ambapo amezungumza na wanachama mbalimbali katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Fidel Castro Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema kutokana na uimara huo hakuna chama kingine mbadala wa Chama Cha Mapinduzi kinachoweza kushuka kwa wananchi nyumba kwa nyumba na kuratibu kero zao kisha kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Dk.Bashiru aliwahakikishia wanachama na viuongozi hao kuwa CCM bado ipo imara na itapata ushindi wa kihistoria mwaka 2020 kwa nchini nzima kuliko ushindi unaopatikana kwa sasa katika uchaguzi mdogo unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
Aliongeza kwamba sababu za kushinda na kusambaratisha upinzani zipo kwani vyama vya upinzani nchini vimekosa muelekeo na ndio maana wanachama wake wanahamia CCM kwa wingi.
Alisema Tanzania inahitaji vyama vya siasa imara vitakavyolinda na kuhubiri misingi ya utaifa na umoja na msikamano wa Tanzania, bila ya kujali tofauti za kisiasa.
Kupitia mkutano huo aliwambia wanachama wa vyama vya upinzania kisiwani Pemba kwamba huu ndio wakati wao wa kujitawala kifikra kwa kujiunga na CCM kwani Chama Cha CUF hakina tena mvuto kwa jamii kutokana na tabia ya unafiki na uongo inayofanywa na viongozi wakuu wa Chama cha CUF.
“Wanachama wa vyama vya upinzani njoo CCM huku tupo shwari na tumekamilika kila idara wala msihofu chochote hakuna mtu yeyote wa kuwagusa, na wale wote waliojiunga na chama chetu leo nahakikishieni kuwa mtafaidika na siasa safi na demokrasia iliyotukuka.
Pia Wana-CCM wenzangu awa wenzetu wanaojiunga na CCM wapokeeni na kuwathamini kwani wamefanya maamuzi sahihi ambayo hawatoweza kuyajutia.”, alisema Dk.Bashiru.
Dk.Bashiru kupitia mkutano huo alitangaza rasmi kuwa Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuvunja ngome zote za upinzani kabla ya mwaka 2020, kutokana na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015/2020.
Alisema dhamira ya tasisi hiyo kwa sasa ni kuendeleza kwa vitendo mambo mema yaliyoasisiwa na vyama vya ukombozi vya ASP na TANU vilivyoungana na kuzaliwa kwa CCM.
Pamoja na hayo aliweka wazi kuwa kila kila mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi anatakiwa kulinda Muungano, Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwani tunu hizo ndio chimbuko la mafanikio yaliyopo hivi sasa.
Kupitia mkutano huo pia Dk.Bashiru aliwapokea wanachama wapya 62 waliotoka chama cha CUF na kujiunga na CCM kisiwani Pemba.
Aliwapongeza wanachama wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kumuamini kasha kupendekeza ateuliwe kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM Tanzania, na akaahidi kuwa atatumia nafasi yake kuleta mageuzi makubwa ya kimaendeleo ndani nan je ya CCM.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla (Mabodi), alisema kazi kubwa ya Chama cha mapinduzi kwa zama za sasa ni kutekeleza kwa vitendo dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya kwa maendeleo ya jamii.
Alisema miradi mbali mbali ya maendeleo iliyotekelezwa kwa ufanisi kisiwani Pemba ikiwemo mfuko wa maendeleo wa TASAF na kuongeza bei ya zao la karafuu ni kutokana na utekelezaji mzuri wa sera za CCM.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba Ndugu Yussuf Ali Juma alisema ndani ya Mkoa huo wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha CCM inashinda kwa ngazi zote katika uchaguzi Mkuu ujao.
Katika ziara hiyo Dk. Bashiru alifuatana na viongozi mbali wa Chama na Jumuiya wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, wajumbe wa halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Makamu Wenyeviti wa Jumuiya pamoja na viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali Zanzibar.